Hapana wakubwa wa dhulma kuliko hao wanao mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa kumnasibisha na mshirika na mwana, na kuzua kuhalalisha na kuharimisha na mengineyo, pasina hoja. Au wanao kanusha Aya, Ishara, za Mwenyezi Mungu zilizo funuliwa katika Vitabu vyake na zinazo onekana katika ulimwengu wake. Hao wanapata hapa duniani sehemu ya aliyo waandikia Mwenyezi Mungu katika riziki, au uhai, au adhabu. Mpaka akiwajia Malaika wa Mauti kuzipokea roho zao, hapo huwaambia kwa kuwasuta: Iko wapi hiyo miungu yenu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu ije kukukingeni na mauti? Nao wajibu: Wametukataa, wametuacha na wametukimbia. Na wajishuhudie wenyewe wakikiri kuwa hakika walikuwa makafiri.