Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu, nalo ni nguo hizi "maaddiy" za kuonekana, za kusitiri utupu, na nguo za "adabiy" zisizo onekana, bali ni za maana, nazo ni Taqwa, Uchamngu, katika kila pahala pa Swala, na kila wakati mnapo fanya ibada. Na jistarehesheni kwa kula na kunywa bila ya kufanya israfu au ubadhirifu, yaani kutumia kwa fujo, katika hayo. Basi msitumie vitu vilivyo harimishwa, wala msipite kiasi cha kiakili katika huko kujistarehesha. Hakika Mwenyezi Mungu hana radhi na wanao tumia kwa fujo.