Na Musa alipo rejea kutoka kuzungumza na Mola Mlezi wake kuja kwa watu wake, naye kakasirika nao kwa vile walivyo muabudu ndama, na amehuzunika kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewatia mtihanini - kwani Mwenyezi Mungu alikwisha mpa khabari ya yale kabla hajarejea - aliwaambia: Kitendo gani kiovu hichi mlicho kitenda baada ya kuondoka kwangu! Mmetangulia kwa kumuabudu ndama msifuate amri ya Mola wenu Mlezi kuwa mningojee, na mkawa hamkuishika ahadi yangu mpaka nikakuleteeni Taurati? Akaziweka zile mbao, na akamuelekea nduguye kwa huzuni kubwa kwa yale aliyo yaona kwa kaumu yake. Akaingia kumvuta ndugu yake kwa kichwa akimbururia kwake kwa wingi wa ghadhabu. Haya ni kuwa alidhani kuwa amefanya taksiri hakuwazuia kufanya walio yafanya! Haarun akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu walipo fanya waliyo yafanya walinidharau na wakanishinda nguvu. Na wakakaribia kuniuwa kwa kuwa niliwakataza wasimuabudu ndama. Basi usiwafurahishe maadui kwa kunitesa mimi, wala usiitakidi kuwa mimi ni mmoja wa wenye kudhulumu, kwani mimi ni mbali nao na dhulma yao. Haarun amemwita Musa kwa kumnasibisha na mama yao, ijapo kuwa hao walikuwa ndugu khalisa, wa baba na mama, kwa sababu huyo mama alikuwa Muumini. Kumtaja yeye ni kuzidi kukumbusha mapenzi.
Musa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nisamehe kwa haya niliyo mfanyia ndugu yangu kabla sijayajua mambo. Na msamehe ndugu yangu ikiwa kakosea katika kushika pahala pangu kwa vizuri. Na tuingize katika eneo la rehema yako, kwani Wewe ndiwe Mwenye rehema nyingi kushinda wote wenye kurehemu.
Hakika wale walio endelea kumfanya ndama kuwa mungu, kama Msamaria na wenziwe, itawafika ghadhabu kubwa kutoka kwa Mola wao Mlezi huko Akhera, na uvunjifu mkubwa katika maisha ya duniani. Na mfano wa malipo hayo ndio tunamlipa kila mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo, na akaabudu kinginecho.
Na wale walio tenda vitendo vibaya vya ukafiri na kuabudu ndama na maasi mengineyo, kisha wakarejea kwa Mwenyezi Mungu baada ya kutenda hayo, na wakamsadiki, basi hakika Mola wako Mlezi baada ya toba yao, ni Mwenye kuwasitiri, na kuwasamehe kwa hayo waliyo kuwa nayo.
Na Musa zilipo muondoka ghadhabu kwa kutoa udhuru nduguye, akazirejea zile mbao alizo ziweka chini akazichukua. Na kwenye hizo mbao umeandikwa uwongofu, na uwongozi, na njia za kupata rehema, kwa wale wanao iogopa ghadhabu ya Mola wao Mlezi.
Kisha Mwenyezi Mungu alimuamrisha awalete baadhi ya jamaa katika kaumu yake wawatakie radhi walio muabudu ndama, na akawapa miadi. Musa akawateuwa katika kaumu yake watu sabiini katika wasio muabudu ndama, nao wakawa wanawawakilisha kaumu yao. Akenda nao mpaka kwenye mlima. Na huko wakamwomba Mwenyezi Mungu awaondolee balaa, na akubali toba ya walio muabudu ndama kati yao. Ikawachukua zilzala (tetemeko) kubwa pahala hapo, wakazimia kwa sababu yake. Na hayo kwa kuwa hawakuwaacha kaumu yao walipo abudu ndama, wala hawakuamrisha mema, wala hawakuwakanya maovu! Musa alipoona yale alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Lau ungeli penda kuwaangamiza ungeli waangamiza kabla hawajaja hapa kwenye miadi, na ukaniangamiza na mimi pia, ili waone hayo Wana wa Israili wasinituhumu kuwa mimi nimewauwa. Basi ewe Mola Mlezi wangu! Usituhiliki kwa walio yafanya wajinga kati yetu. Kwani hii balaa ya kuabudu ndama haikuwa ila ni majaribio yaliyo toka kwako. Wewe unampoteza unaye taka apotee katika hao wanao ishika njia ya shari, na unawahidi (unawaonoza) unaye taka ahidike. Wewe ndiye mwenye kusema: Nitawaandikia wenye kujikinga na ukafiri na maasi katika kaumu yako, na akatoa Zaka iliyo faridhiwa, na Mwenye kusamehe madhambi.