Ametukuka, na amezidi baraka zake Mwenye kumiliki peke yake uwezo wa kuendesha mambo ya viumbe vyote. Na Yeye, juu ya kila kitu, anao uwezo ulio timia.
Ambaye ndiye aliye umba mauti na uhai kwa makusudio anayo yataka Yeye, ili akufanyieni mtihani ni yupi katika nyinyi anaye fanya vitendo sawa, na mwenye niya safi. Na Yeye ni Mwenye kushinda, wala hashindiki kwa kitu, Mwenye msamaha kwa wenye upungufu.
Yeye ndiye aliye zizua mbingu saba zilizo pandana kwa mpango mmoja sawa sawa. Huoni tafauti yoyote katika uundaji wa Mwenyezi Mungu, ambaye rehema yake imeenea kwenye viumbe vyake vyote. Basi hebu tazama tena, unaona khitilafu yoyote?
Kisha tazama tena, na tena! Jicho lako linakurejea mwenyewe bila ya kugundua aibu yoyote, nalo limechoka.
Na hakika Sisi tumeipamba mbingu hii ya karibu, unayo iona kwa macho, tumeipamba kwa nyota zinazo ng'aa. Na tumefanya katika hizo vimondo vya kuwapopolea mashetani; na Akhera tumewaandalia adhabu ya moto unao waka. Mbingu ni kila kilicho juu yetu kikatufunika. Amesema Ibn Sayyidih: Hiyo ni bahari ya anga na vyombo vyote viliomo ndani yake na vimondo. Na sura wanayo iona wakaazi wa duniani katika masiku yaliyo safi ni kama qubba la kibuluu lilio pambwa kwa nyota na sayari kama kwamba ni taa, kama unavyo ziona nyota za mkia, au vimondo, vinakwenda angani vikiungua huko juu ya ardhi. Na hilo qubba la kibuluu si chochote ila ni matokeo ya mwangaza wa jua na nyota pamoja na takataka za vumbi zinazo ning'inia katika hewa, na sehemu za hewa molecules zinazo tawanyika. Haya mbali na yanayo onekana katika mwangaza nafsi yake ambayo huipamba mbingu hii ya karibu, kama vile zile rangi nzuri nzuri za wakati wa kuchwa jua, au wakati wa kuchomoza jua alfajiri, na mianga ya njia za nyota, miangaza ya kaskazini, na miangaza ya katika sehema za Polar regions. Na hayo yote yanayo onekana ni matokeo ya kuingiliana mwanga pamoja na funiko la anga la ardhi na uwanja wake wa smaku, magnetic field.
Na kwa ajili ya wasio muamini Mola wao Mlezi tumewawekea adhabu ya Jahannamu. Na huo ndio mwisho muovu kweli kwao.
Unakaribia kukatika na kutawanyika kwa wingi wa kuwaghadhibikia. Kila likitumbukizwa kundi mojapo kati yao walinzi wake huwauliza kwa kuwakejeli: Kwani hakukujieni Mtume kukuhadharisheni na mkutano wa siku hii ya leo?
Na wao watajibu: Ametujia mwonyaji, lakini sisi tulimkanusha tukamwambia mwongo, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakukuteremshia chochote wewe wala Mitume wenginewe. Nyinyi mnao dai Utume si chochote ila ni watu walio potoka, na mko mbali na haki.
Na watasema: Lau kuwa tulikuwa tunasikia kama inavyo faa asikie mwenye kutaka ukweli wa mambo, au tunafikiri tunayo itiwa, tusinge kuwa miongoni mwa watu wa Motoni.
Hakika wenye kumkhofu Mola wao Mlezi, na hali wao hawamwoni, watafutiwa madhambi yao, na watapata thawabu kubwa kwa mema yao.