Hivyo ndivyo ilivyo kuwa hali ya mataifa yote kwa Mitume wao. Hakuja Mtume kwa watu wa kabla ya kaumu yako ila walimwita: Mchawi au mwendawazimu.
Sitaki kwao riziki, kwani Mimi si mhitaji kwa walimwengu wote; wala sitaki wanilishe, kwani Mimi ndiye ninaye lisha, wala silishwi.
Hakika hao walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na kukanusha wana fungu lao la adhabu mfano wa fungu la wenzao katika kaumu zilizo kwisha pita. Basi wasifanye haraka kuhimiza adhabu ishuke kabla ya wakati wake.