Na hao makafiri wa kaumu yako wakikukadhabisha kwa uwongofu ulio waletea, basi wewe wastahamilie. Kwani Mitume wa kabla yako walikwisha kadhibishwa vile vile, na wakavumilia kwa walivyo kadhibishwa mpaka wakashinda. Na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu, juu ya mambo ya kufufuliwa, na malipo, na ushindi, ni haki ya kweli. Basi msiache dunia ikakukhadaini na Akhera. Wala Shetani akakukhadaini mkaacha kuwafuata Mitume, na akakupeni tamaa kuwa mtasamehewa na hali huku mnaendelea na maasi.
Hakika Shetani ni adui yenu wa kale, msikhadaike kwa ahadi zake. Nanyi mchukulieni kuwa ni adui yenu. Kwani hakika yeye anawaita wafwasi wake wapate kuwa watu wa Moto uwakao kwa nguvu, na wala hawaitii kwa jenginelo.
Wanao mkufuru Mwenyezi Mungu na Mitume wake watapata adhabu kali. Na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakatenda mema watapewa kutokana na Mwenyezi Mungu kusamehewa madhambi yao, na ujira mkubwa kwa vitendo vyao.
Wamekuwa hawatambui? Je! Yule ambaye Shetani kampambia vitendo vyake viovu na mwenyewe akaona ni vizuri, ni kama aliye hidika kwa uwongofu wa Mwenyezi Mungu na akaliona jema kuwa ni jema, na uovu akauona kuwa ni uovu? Kwani hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye katika wanao khiari njia ya upotovu, wakaiona ndiyo njia ya kuifuata. Na humhidi amtakaye miongoni mwa walio ikhiari njia ya hidaya kuwa ndiyo njia ya kuifuata. Basi usiihiliki nafsi yako kwa kuwasikitikia wapotovu na kuwaonea huruma. Hakika Mwenyezi Mungu anajua uovu wautendao, naye atawalipa kwa hayo.
Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye zituma pepo ziyatimue mawingu yaliyo rindika kwa mvuke wa maji. Tena tukayasukuma hayo mawingu mpaka kwenye nchi yenye ukame, tukaihuisha ardhi yake baada ya kuwa ilikuwa imekufa. Kama tunavyo itoa mimea katika ardhi, basi hali kadhaalika tutawatoa maiti makaburini Siku ya Kiyama. Rejea maoni ya ki-ilimu juu ya Aya 57 katika Surat Al Aa'raaf.
Mwenye kutaka utukufu na nguvu na akazitafute kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu. Kwani Yeye ndiye Mwenye nguvu zote. Kumwendea Yeye ndio linapanda neno jema. Na Mwenyezi Mungu huinyanyua a'mali njema na akaipokea. Na wale wanao wapangia Waumini vitimbi vya kuwadhuru watapata adhabu iliyo kali. Na hizo njama zao zitafisidika, hazito leta hayo waliyo yakusudia, wala hazileti natija yoyote.
Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kwani ndivyo hivyo alivyo muumba baba yenu Adam. Kisha akakuumbeni kutokana na tone ya manii, nayo ni maji yanayo miminwa katika tumbo la uzazi, nayo pia ni katika chakula kinacho toka kwenye udongo. Kisha akakufanyeni waume na wake. Wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai ila kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wala hauongezwi umri wa mtu yeyote, wala haupunguzwi ila husajiliwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni sahali, mepesi.