Katika Siku hiyo makafiri hawatokingwa na mali yao na yangawa mengi vipi, wala na watoto wao na wangawa wengi vipi. Hayo yote yatakuwa ndio kuni za Moto za kuwateketeza wenyewe.
Na hali ya hao ni kama hali ya kaumu ya Firauni walio kuwa na inda kabla yao. Walizikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu juu ya kuwa zilikuwa ziwazi kabisa. Basi Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya madhambi waliyo yatenda. Na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Ewe Nabii! Waambie hawa walio kufuru: Bila ya shaka nyinyi mtashindwa hapa duniani, na kesho Akhera mtaadhibiwa. Na Jahannamu ndio itakuwa tandiko lenu la kulalia; na ovu lilioje tandiko hilo!
Ilikuwa Ishara wazi na mazingatio yaliyo dhaahiri katika makundi mawili ya wapiganaji walipo pambana siku ya Badri. Kundi moja, hilo la Waumini, likipigana kwa ajili ya kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu na kueneza Haki. Na kundi la pili, hilo la makafiri, likipigania pumbao na matamanio. Ikawa, basi, Mwenyezi Mungu katika kuwaunga mkono Waumini aliwafanya wale makafiri wawaone Waumini idadi yao mara mbili kuliko walivyo. Kwa hivyo makafiri wakaingiwa na khofu nyoyoni mwao wakaemewa. Na Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Katika haya, hakika, pana mazingatio kwa wenye nadhari iliyo ongoka isiyo kengeuka na kuiacha Haki.
Wanaadamu wameumbwa kuwa wanapenda matamanio ya vitu kama wanawake, wana, na wingi wa madhahabu na fedha, na farasi wazuri wazuri walio fundishika, na mifugo kama ngamia, ng'ombe, mbuzi, kondoo, na kadhaalika mashamba makubwa. Lakini yote hayo ni starehe na kwa matumizi ya uhai huu wa duniani wenye kupita na kuondoka. Na hayo si chochote si lolote ukilinganisha na hisani anayo wafanyia Mwenyezi Mungu waja wake wanao pigania jihadi katika Njia yake watakapo rejea kwake Yeye Akhera.
Ewe Nabii! Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo yote mliyo pambiwa duniani? Kwa wale wachamngu wamewekewa malipo ya dhamana kwa Mola wao Mlezi, nayo ni Bustani zipitazo mito chini ya vivuli vya miti. Humo watastarehe kwa maisha mazuri wala hawatoingiliwa na khofu ya kuwa neema hiyo itaondoka, kwani wamekwisha katibiwa kuwa humo watabaki daima milele. Watakuwamo humo wake walio t'ahirika, wamesafika na kila ila ya wanawake wa kidunia. Na juu ya yote hayo, watapata Radhi ya Mwenyezi Mungu ambayo wataihisi chini ya kivuli chake kuwa ndiyo Neema kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali za waja wake; hapana jambo linalo fichikana kwake, hawana siri asiyo ijua Yeye.