Ewe Muaminifu! Watajie pale walipo ingia kwake, naye akawaogopa. Wao wakamwambia: Amani kwako, na tulia! Yeye akasema: Sisi tunakuogopeni, kwani mmetujia kwa ghafla, sio wakati wa dasturi wa kufika wageni, na hatujui mna nini!
Wakasema: Usiogope, na tuwa moyo! Kwani tunakubashiria mwana, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atampa siku zijazo za uhai wake ilimu kubwa. Inaonyesha hapa kuwa bishara hii si ya Ismail a.s. Kwani Ismail alikuwa kesha zaliwa, naye na mama yake Haajir walikuwa wapo Makka. Bishara hii ni ya Ibrahim na mkewe, basi kwa hivyo ni ya Is-haq mwana wa Ibrahim na Sara.
Akasema: Vipi mnanibashiria mtoto na hali mimi nimekwisha patikana na udhaifu wa ukongwe. Kwa njia gani, basi, mnanibashiria jambo hili la ajabu?
Wakasema: Sisi tunakubashiria jambo lilio thibiti, ambalo halina shaka kabisa. Basi usiwe katika wanao kata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Ibrahim akasema: Mimi sikati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu ila walio potea wasio utambua utukufu wake na uwezo wake.
Wakasema hakika sisi tumetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu walio fanya ukhalifu katika Haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya Nabii wao, na haki ya nafsi zao wenyewe. Ukhalifu ndio mtindo wao. Watu wenyewe ni kaumu ya Luut'i. Basi tutawateketeza.
Wakasema: Usituogope, kwani hatukukujia kwa unalo liogopa, bali tumekujia kwa jambo la kukufurahisha, nalo ni kuwateremshia adhabu hawa watu wako walio kukadhibisha na wakawa wanaitilia shaka hiyo adhabu au wanaikanya.
Ilivyo kuwa adhabu itawateremkia, basi wewe na ahli zako mlio andikiwa kuokoka, tokeni baada ya kwisha ingia usiku.
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la alimfunulia Luut'i kwa kumwambia: Sisi tumewahukumia na kuwakadiria wakosefu kuteketea. Watang'olewa itapoingia asubuhi, wala hatobaki hata mmoja wao.