Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na kutajwa kwa wema, ni kwa Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi, na akaumba, kwa kudra yake, giza na mwangaza, kwa manufaa ya waja wake, na kuambatana na hikima yake. Tena pamoja na neema zote hizi nzuri hawa makafiri wanakwenda mshirikisha Mwenyezi Mungu, na wakawafanya wengineo ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada!! Aya hii tukufu ni ishara ya ubora wa kuumba, na ubora wa kuumba unaonyesha Umoja na Upweke wa Mwenye kuumba na utukufu wake. Kwani mbingu na nyota zake, na sayari zake, na jua, na mwezi - vyote hivyo ni ushahidi wa Umoja wake. Na ardhi na viliomo ndani yake, navyo ni wanyama, mimea na visio na uhai, na milima na mabonde, na rutuba na ukame, na viliomo chini ya ardhi maadeni magumu na yanayo tiririka, na bahari na viliomo ndani yake kama lulu na vilio hai - vyote hivyo vinaonyesha Umoja wa Mwenye kuumba. Na giza la kila namna, kama giza la jabali, na bahari, na mapango, na ukungu ulio funga moja kwa moja hata mtu akiutoa mkono wake anakaribia kuwa asiouone - pia vyote hivyo vinaonyesha ujuzi usio kuwa na mfano, wa kuanzisha kuumba, wa Mwenyezi Mungu Aliye viumba. Hali kadhaalika nuru, na sababu zake mbali mbali, kama nuru ya jua, na mwangaza wa mwezi, na mwangaza wa nyota ... vyote hivyo vinaonyesha uanzishaji wa Mwenyezi Mungu wa kuumba bila ya kiigizo.
Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuanzeni kwa kukuumbeni kutokana na udongo. Kisha akamkadiria kila mmoja wenu ana zama maalumu za uhai, kisha uhai huo unakwisha kwa kufa. Na muda maalumu ulio wekwa wa kufufuliwa kutoka kaburini uko kwake Yeye pekee. Kisha tena enyi makafiri! Mnabisha uwezo wa Mwenyezi Mungu kufufua, na kustahiki kwake peke yake kuabudiwa?
Na ni Yeye peke yake anaye stahiki kuabudiwa katika mbingu na katika ardhi. Anajua kila mnacho kificha na mnacho kionyesha. Na anajua yote mnayo yatenda, Naye atakulipeni kwa hayo.
Wala washirikina hawaletewi ishara yoyote katika ishara za Muumbaji wao zinazo shuhudia Umoja wake na ukweli wa Mitume wake, ila wao huikataa na kuibeza ishara hiyo, wala hawaizingatii, wala hawaitii maanani!
Wao wameikanusha Qur'ani ilipo wajia, na ilhali hiyo ni Haki isiyo changanyika na upotovu! Basi yatawapata mateso ya duniani, na adhabu ya Akhera, kama ilivyo eleza Qur'ani. Na hapo utawabainikia ukweli wa onyo lake walilo kuwa wakilifanyia maskhara.
Hivyo wao hawajui kuwa kabla yao tuliwaangamiza umati kwa umati? Tuliwapa sababu za nguvu na kuselelea katika nchi tusizo pata kukupeni nyinyi, enyi makafiri. Na tuliwakunjulia riziki na starehe. Tukawateremshia mvua nyingi iliyo wanufaisha katika maisha yao, na tukaifanya mito inapita chini ya majumba yao ya fakhari. Nao basi wasishukuru kwa neema hizo. Kwa hivyo tukawaangamiza kwa sababu ya ushirikina wao na kukithiri dhambi zao. Baada yao tukawaleta watu wengine walio bora kuliko wao.
Ewe Nabii! Hata tungeli kuteremshia dalili ya ujumbe wako iliyo andikwa katika karatasi, na wao wakaiona kwa macho yao, na wakahakikisha kwa kuiwekea mikono yao juu yake, basi pia wangeli sema kwa chuki tu: Hichi tunacho kigusa si chochote ila ni uchawi tu.
Tena wanasema: Tunataka Mwenyezi Mungu amteremshia Malaika huyu anaye dai Utume amsadikishe! Na lau kuwa Sisi tungeli waitikia hilo ombi lao, tukampeleka Malaika kama walivyo toa shauri, kisha wakafanya inda yao wasimuamini, basi amri ya kuwaangamiza ingesha pitishwa, tena hao wasinge pewa muhula hata chembe.