Fungu la mume ni nusu ya alicho acha mke ikiwa huyo mke hakuacha mtoto kutokana na mume huyo au mwenginewe. Akiwa huyo mke ana mtoto, basi mumewe atapata robo baada ya kutolewa wasia aliye uusia huyo mwanamke au kulipwa deni lake. Na fungu la mke au wake ni robo ya alicho acha mume ikiwa hakuacha mtoto kwa wake hao au wenginewe. Akiwa anaye mwana kutokana na hao au wake wenginewe basi mke huyu au wake hawa watapata thumni ya tirka baada ya wasia alio usia au deni. Na mwana wa mwana, yaani mjukuu, ni kama mwana katika haya yaliyo tangulia. Na akiwa maiti ni mwanamume au mwanamke, naye hana mwana wala mzazi, na kamwacha ndugu mume kwa mama, au ndugu wawili wa kike kwa mama, basi kila mmoja wao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita. Na wakiwa wengi kuliko hivyo watashirikiana katika thuluthi, watagawana sawa sawa wanaume na wanawake kwa mujibu wa ushirika, baada ya kulipa madeni yaliyo kuwa juu yake, na kutimiza wasia ambao haudhuru urithi, nao ni wasia usio pindukia thuluthi iliyo baki baada ya kulipa madeni. Basi, enyi Waumini! Jilazimisheni kufuata aliyo kuusieni Mwenyezi Mungu; kwani Yeye hakika ni Mwenye kujua vyema nani miongoni mwenu anaye dhulumu na nani anaye fanya uadilifu, Yeye ni Mpole hafanyi haraka kutoa adhabu.