Harufi hizi zimeanzia baadhi ya Sura kuashiria kuwa Qur'ani ni muujiza ulio tungwa na harufi kama harufi wanazo zitumia Waarabu katika maneno yao. Na juu ya hayo wao wameshindwa kuleta mfano wake. Na pia ni kwa ajili ya kuzindua watu wasikilize na watege sikio. Na washirikina walikuwa wamewafikiana kuwa wawe wanaropokwa maneno ya upuuzi tu ikisomwa Qur'ani wala wasiisikilize.
Hao ndio wanao timiza Swala kwa njia ya ukamilifu kabisa, na wanawapa Zaka wanao istahiki; na wao wanayaamini maisha ya Akhera kwa imani yenye nguvu kabisa.
Hao Waumini wanao tenda vyema vitendo vyao, wametua kwenye Uwongofu ulio wajia kutokana na Mola wao Mlezi. Na hao tu - si wengineo - ndio wenye kufuzu kikweli.
Na miongoni mwa watu wapo ambao hununua maneno ya uwongo wawasimulie watu wapate kuwatenga na Uislamu na Qur'ani kwa kutojua dhambi zilio juu yao, na wanaifanyia maskhara Dini ya Mwenyezi Mungu na Ufunuo wake. Watendayo hayo watapata adhabu ya kuwatia unyonge na kuwadhalilisha.
Na mpotovu kama huyu akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu huzipuuza kwa kiburi. Hali yake kwa haya ni hali ya ambaye hasikii, kama kwamba ana uziwi katika masikio yake. Basi mwonye kuwa hakika Mwenyezi Mungu amemuandalia adhabu yenye machungu makali.
Watabaki humo daima dawamu; Mwenyezi Mungu amewaahidi ahadi isiyo vunjika. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mshindi wa kila kitu, Mwenye hikima katika maneno yake na vitendo vyake.
Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu zisio na nguzo za nyinyi kuziona. Na juu ya ardhi ameweka milima iliyo simama imara, ili ardhi isikutingisheni. Na humo katika ardhi ametawanya kila namna ya wanyama wanao tambaa na kwenda. Na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha mimea ya kila namna nzuri yenye manufaa katika ardhi. Rejea uangalie maelezo ya kisayansi juu ya Aya 2, Sura ya Ar-Raa'd.
Hivi viumbe vya Mwenyezi Mungu vipo mbele yenu, basi hebu nionyesheni walicho umba hao mnao wafanya ni miungu badala yake Yeye hata wawe ni washirika wake! Bali madhaalimu - kwa ushirikina wao - wamo katika upotovu ulio wazi.