Ewe Nabii! Kumbuka na utaje pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi madhbuti kwa Watu wa Kitabu, kuwa wayaeleze wazi maana ya Kitabu chao, na wala wasiwafiche watu chochote, na wao wakakitupilia mbali nyuma ya migongo yao, na badala yake wakatafuta starehe za dunia. Na starehe za dunia kama zitakavyo kuwa ni kitu chenye thamani duni kabisa kulinganisha na uwongofu na uwongozi. Ama wamejua kutenda uovu! (Hayo yalikuwa zamani na bado yanaendelea. Kuficha na kugeuza na kupotosha Biblia hakusiti. Vipo vitabu vyao vinavyo itwa "Apokrifa", maana yake "Vilivyo fichwa", kwa kuwa hivyo ni marfuku visisomwe ila na mapadri tu, na vingine vimeteketezwa. Miongoni mwa hivyo ni Injili ya Barnaba.)