Kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mema hakutowakinga hata chembe na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuja tu, kama si leo kesho. Wala hapana kheri katika neema ambayo khatima yake ni adhabu.
Basi wewe muelekee Mwenyezi Mungu ukiendelea na usafi wako wa ibada, wala usishughulike na fisadi za madai ya washirikina na mwendo wao muovu. Na hivi kutakiwa Mtume s.a.w. awe na ikhlasi ya namna hii ni wito kwa jamii ya watu waliomo katika umma wake.
Hakika Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kusikia dua zako na dhikri zako, ndiye Mjuzi wa kujua niya yako na vitendo vyako. Ni kama kwamba Subhanahu anamwambia: Usichukue taklifu kubwa bila ya kiasi katika mashaka ya ibada, kwani uyatendayo yote nayaona na nayasikia Mimi.
Wanamteremkia kila mwenye kubeba dhambi za namna mbaya kabisa za uwongo, na madhambi ya kuchusha kabisa. Nao ni hao makohani mafisadi ambao tabia zao na tabia za Mashetani ni jinsi moja na zimewafikiana.
Makafiri wanasema: Hii Qur'ani ni mashairi, na Muhammad ni mtungaji mashairi. Mwenyezi Mungu ameyavunja haya kwa kuthibitisha kuwa hakika Qur'ani imejaa hikima na hukumu. Mpango wake unapingana na mpango wa mashairi ambao unategemea juu ya kweli na uwongo. Na amebainisha kwamba hali ya Muhammad s.a.w. inapingana na hali ya watungaji mashairi. Yeye anasema kwa hikima, wao wanasema kwa udanganyifu. Na hii ndiyo hali ya wengi katika watungaji mashairi.
Lakini walio hidika kwa hidaya ya Mwenyezi Mungu, na wakatenda mema mpaka zikatua katika nafsi zao sifa bora, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi mpaka ikathibiti khofu katika nyoyo zao, hawa basi huyafanya mashairi kama dawa ilio sibu kwa ugonjwa wake. Na hupambana kwa ajili ya kuiwania Dini yao na kusimamisha Haki, inapo kuwa Haki inafanyiwa jeuri. Na walio dhulumu nafsi zao kwa shirki na kumkejeli Mtume kwa mashairi, watatafuta wapi pa kuikimbia shari na hilaki wanayo iendea.