Wala mimi sitaki kwenu ujira kwa uwongofu na uwongozi ninao kuitieni. Sina ujira ila kwa Mwenye kumiliki viumbe vyote na Mlezi wao.
Lut'i alisema: Nyinyi mnastarehea kuwaingilia wanaume mkaacha wanawake? Kwa hayo anakusudia kuyakanya yale waliyo yazoea ya vitendo vichafu. "Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?" Yaani kazi ya liwat'i, ambayo tangu asli yake ni ukosefu muovu, unao chusha hata kuusikia, kinyume na maumbile, unao mteremsha mwanaadamu chini kabisa. Na lau kuwa unaenea basi huharibu sunna ya kuoa, nayo ni sunna ya maumbile, hata uzazi ukatike na ulimwengu usite kuendelea. Na kwa liwat'i huenea maradhi kama yanavyo enea kwa uzinzi kama tego, kisonono, donda ndugu, maradhi ya ngozi kama ukurutu, na hutokea ishara za kudhoofika nyama za nyuma hata ikawa mtu hawezi kujizuia kutokwa na choo ovyo. Na nyuma kwake mtu huchanua kukawa kama mdomo wa tarumbeta. Na huko nyuma hujaa vijidudu vya maradhi na hivyo humuambukiza mwenye kumuingilia na yeye hivyo vijidudu vikenda mletea maradhi mengine ya njia za mkojo. Na huenda huyo mwenye kufanywa mambo hayo akawa mpumbavu hafai kitu, ikiwa kaanza tangu utotoni. Na huenda akajidai kuonesha ujanadume mwingi kuliko kiasi kwa kutaka kuficha upungufu wake wa uume. (Karibuni imedhihiri kuwa maradhi ya khatari kabisa ya AIDS [Ukimwi] yameenea zaidi sana kwa watendao kitendo hichi na watumiao madawa ya ulevi, ijapo kuwa na wazinzi nao hupata!). Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameukemea ukosefu huu katika Aya kadhaa wa kadhaa, na akabainisha hikima ya Mwenye kuhukumu kwa kuharimisha huku, kwa kusema: " Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume? Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!"
Na mnaacha aliyo kuumbieni Mwenyezi Mungu ya kustarehe na wake zenu walio halali yenu? Ama hakika nyinyi ni watu mlio pindukia mipaka ya udhalimu katika kufanya maasi.
Walikasirika kwa kule kuwakataza na kuwakemea kwa sababu ya jambo ovu na wakasema: Kama hukuacha kutukebehi tutakutoa mji kwa izara kubwa.
Na Mwenyezi Mungu aliwateremshia wale watu wapotovu mawe kutoka mbinguni, yakawateketeza. Na ilikuwa mvua ya kutisha kwa wingi wake na namna yake. Basi mvua ovu ya walio kwisha onywa ni mvua hiyo, kwani iliteremka kwa uangamizi mkubwa mno!
Hakika adhabu ile iliyo wateremkia watu wale hapana shaka ni hoja yenye kuonyesha utimilivu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Wala si wengi katika watu wako wenye kusadiki hayo.
Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kusifika kwa rehema iliyo kamilika. Huwapa adhabu watendao dhambi, na huwalipa wema Waumini.
Hichi kisa cha Shuaibu pamoja na Watu wa Al Aykat, Machakani, nao ni msitu wenye miti mizuri, karibu na Madian. Kikundi cha watu waliteremkia hapo na wakakaa. Mwenyezi Mungu akawapelekea Shuaibu kama alivyo wapelekea watu wa Madian. Wakamkadhibisha katika wito wake. Na kwa hivi wakawa wamekanusha risala za Mitume wote.
Na mimi kwa hivi kukuongozeni na kukufunzeni sikutakini ujira wowote. Mimi sina malipo kaamili kwa sababu ya kazi yangu ila kutokana na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Shuaibu akawaamrisha kutimiza vipimo kwa ukamilifu wanapo pima, kwani ilikuwa ada yao kupunguza kwa pishi na mizani, kupunguza haki za watu kwa kuwapunja na kuwapimia kasoro.
Wala msiwapunguzie watu haki zao, wala msipite katika nchi mkifisidi kwa kuuwa, na uharamia, na kufanya madhambi, na kufuata pumbao.