Watapenda, na watatamani sana makafiri wanao zikanya Aya za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, watapo ona adhabu ya Siku ya Kiyama, lau kuwa walisilimu walipo kuwapo duniani, na wakafuata kwa ikhlasi Dini ya Mwenyezi Mungu.
Lakini sasa wamo katika kughafilika, hawazingatii adhabu itakayo wapata Akhera! Basi ukisha wafikishia ujumbe wako, na ukawaonya, waachilie mbali. Wao hawana hamu ila kula, na kustarehe kwa ladha za dunia. Tamaa ya uwongo inawazuga. Na hakika bila ya shaka yoyote watakuja jua yatakayo wapata pale watapo yaona kwa macho yao Siku ya Kiyama.
Na ikiwa wao wanataka wateremshiwe adhabu ya duniani, kama Mwenyezi Mungu alivyo wateketeza walio kuwa kabla yao, basi wajue kuwa Mwenyezi Mungu hauteketezi mji wowote ila kwa wakati wake maalumu.
Na uovu wa hali yao na wingi wa kughafilika kwao hata imefika hadi kumuita Nabii wao kwa kejeli wakisema: Ewe uliye teremshiwa Kitabu cha kukumbusha! Hapana shaka kuwa wewe una wazimu moja kwa moja! Huko kumuita kuwa ndiye aliye teremshiwa Ukumbusho, yaani Mawaidha, hakukuwa ila ni kwa kejeli tu, kumfanyia maskhara.
Na hadi ya ukafiri wao walizidisha juu ya matusi hayo na kejeli kwa kusema: Laiti badala ya hicho Kitabu kilicho teremshwa ungeli tuletea Malaika wakawa ndio hoja yenyewe, kama wewe ni msema kweli miongoni mwa wenye kusema kweli!
Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka neno lake aliwajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika ila huwa pamoja nao Haki ya nguvu yenye kuthibiti ambayo haina njia ya kuikataa. Basi wakiikanya huwa tena hawapewi muhula wowote, bali huteremshiwa adhabu ya hapa hapa duniani hapo hapo!
Na hakika, kwa ajili ya kuwa Wito wa Nabii huyu kwendea Haki udumu mpaka Siku ya Kiyama, hatuwateremshi Malaika, bali tumewateremshia hii Qur'ani ambayo kukumbusha kwake kunaendelea daima dawamu. Na Sisi ndio wenye kuilinda isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko yoyote mpaka kusimama Kiyama.
Na ewe Mtume Muaminifu! Usihuzunike; kwani Sisi tuliwatuma Mitume kabla yako kwa mataifa ambao wameshikilia upotovu kama hao walivyo shikilia. Na wao wamepita pamoja na wa kale walio teketezwa kwa ukafiri wao!
Wala mtindo wao hao walio watangulia kwa kushikilia upotovu haukuwa ila kuwafanyia maskhara Mitume wao, Mtume baada ya Mtume, kama wanavyo kufanyia kejeli wewe! Huo ndio mtindo wa wapotovu!
Kama tulivyo itia Qur'ani katika nyoyo za Waumini ikaingiza mwangaza, basi kadhaalika tumeingiza upotovu katika nyoyo za walio pigwa muhuri wa ukosefu; hali ya katika nyoyo zao ikawa kinyume cha hayo. Upotovu ukatia mizizi katika roho zao.
Wakhalifu hao hawaamini. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa muhula mpaka waione adhabu chungu ya Siku ya Kiyama ndio kama ulivyo kwisha tangulia.
Watu hao wanataka wateremshiwe Malaika. Ewe Nabii! Usidhani kuwa ndio wataamini wakiteremshiwa. Bali hata tungeli wafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda huko wakaona maajabu yaliyoko, na wakawaona Malaika,
Bado wasingeli amini, na wangesema: Macho yetu yamefumbwa tusione, na yamefunikwa. Bali hayo si lolote ila ni uchawi tu, tumerogwa! Basi hapana faida ya ishara yoyote maadamu nyoyo zao zimeenea ukafiri.