Na wajue watu hawa kuwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na neema zake, na ujuzi wake, umeenea kila kitu. Basi hapana mnyama anaye furukuta katika ardhi ila Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake kesha mtengenezea riziki yake inayo wafikiana naye katika hali mbali mbali. Naye anajua anakaa wapi katika hali ya uhai wake, na pahala atapo wekwa wakati wa kufa kwake! Kila kitu katika hayo kimekwisha dhibitiwa kwake Subhanahu katika Kitabu chenye kuweka wazi hali zote ziliomo.
Na Mwenyezi Mungu kaziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake katika siku sita. Na kabla ya hapo palikuwa hapana chochote zaidi kuliko ulimwengu wa maji, na juu yake A'rshi, Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameumba ulimwengu wote huu ili adhihirishe kwa kukujaribuni hali zenu, enyi watu, atokeze kati yenu anaye mkubali Mwenyezi Mungu kwa ut'iifu na vitendo vyema, na nani anaye yaacha hayo...Na juu ya uwezo huu wa kuumba, ukiwaambia kwa yakini: Nyinyi mtafufuliwa kutoka makaburini kwenu, na kwamba wao wameumbwa ili wafe na wafufuliwe, wao mbio mbio wanakurudi kwa mkazo kuwa haya mliyo kuja nayo hayana ukweli wowote! Wala hayo si chochote ila ni kama uchawi ulio wazi wa kuchezea akili tu.
Ilivyo kuwa hikima yetu ni kuakhirisha adhabu ya ukafiri wao hapa duniani mpaka wakati tuliyo uweka, nao ni Siku ya Kiyama, wao husema kwa kejeli: Nini kinacho mzuia hivi sasa? Na ailete hiyo adhabu ikiwa anasema kweli katika hiyo ahadi yake! Basi nawajue hao kwamba adhabu itakuja tu bila ya muhali. Na itapo wajia hawatapata kuokoka, na itawazunguka kwa sababu ya kejeli zao na kutaka kuvunja hishima.
Na katika tabia za binaadamu ni kujizamisha mwenyewe katika hali aliyo nayo. Basi tukimpa baadhi ya neema na rehema, kama vile afya nzuri, na ukunjufu wa riziki, kisha baadae tukamwondolea neema hizo, kwa mujibu wa mipango yetu, yeye hupita mipaka katika kukata tamaa kuwa neema hiyo haitorudi tena; na akapita mipaka katika kuzikufuru neema nyengine ambazo bado angali anastarehe nazo.
Na tukimpa neema baada ya shida aliyo kuwa nayo yeye husema: Shida zangu zote zimekwisha niondokea, wala hazitarudi tena! Na hayo humpelekea upeo wa kufurahikia starehe za dunia, na kujifakhirisha bila ya kiasi. Moyo wake huwa umeshughulika, usimshukuru Mola wake Mlezi! Hii ndiyo hali ya binaadamu wengi, wanababaika baina ya kukata tamaa na kujitapa!
Na aibu hii hawaachi kuwa nayo ila wale wanao subiri wakati wa dhiki, na wakatenda mema wakati wa faraji na shida. Hawa watasamehewa dhambi zao, na watapata ujira mkubwa kwa vitendo vyao vyema.
Ewe Nabii! Usijaribu kutaka kuwaridhi washirikina, kwani hao hawaamini. Na huenda ukijaribu kutaka kuwaridhi ukaacha kusoma baadhi ya uliyo letewa Wahyi, katika yale wasiyo penda wao kuyasikia, kama vile kudharauliwa baadhi ya miungu yao, kwa kukhofu kuwa wasije wakakejeli! Na huenda pengine ukahisi dhiki unapo wasomea, kwa kuwa wao wanataka Mwenyezi Mungu akuteremshie khazina ustarehe nayo kama wafalme, au waje nawe malaika watwambie ukweli wake! Basi, ewe Nabii! Usizibali inadi zao. Kwani wewe si chochote ila ni mwonyaji na mhadharishaji wa adhabu za Mwenyezi Mungu kwa anaye kwenda kinyume na amri yake. Nawe hayo umefanya, basi jipumzishe nafsi yako nao. Na jua kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuangalia na kulinda kila kitu. Naye atawafanyia kama wanavyo stahiki.