Na kwa majaribio kama haya ambayo ndio ada yetu kuyatenda, tukawafanyia mtihani walio takabari kwa kuwatanguliza wanyonge wawe mbele kusilimu; wapate kusema wenye kiburi, wanao pinga, wakifanya kejeli: Hivyo ni hawa mafakiri ndio alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwetu sote kwa kuwapa hiyo kheri aliyo waahidi Muhammad? Hakika hawa mafakiri wanaijua neema ya Mwenyezi Mungu juu yao kwa kuwapa tawfiki ya kuifikia Imani, na kwa hivyo wanamshukuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua zaidi nani anashukuru fadhila yake na neema yake.
Na wakikujia wanao isadiki Qur'ani waambie kwa kuwahishimu: Assalamu Alaikum, Amani juu yenu. Nakubashirieni rehema kunjufu ya Mwenyezi Mungu, ambayo amejilazimisha Yeye Mwenyewe, kwa fadhila yake, na ambayo inahukumu kuwa yeyote katika nyinyi akitenda ubaya bila ya kuzingatia matokeo yake, kisha akarejea kwa Mwenyezi Mungu naye amejuta, ametubu, na akatengeneza a'mali zake, basi Mwenyezi Mungu atamghufiria, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira, na mkunjufu wa rehema.
Na kwa mfano wa bayana hiyo iliyo wazi, tunaweka wazi dalili mbali mbali, ipate kudhihiri njia ya Haki wanayo ipitia Waumini, na ibainishe njia ya upotovu wanayo ipitia makafiri.
Ewe Nabii! Waambie hawa makafiri: Hakika Mwenyezi Mungu amenikataza kuwaabudu hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Basi mimi sifuati matamanio yenu. Kwani nikikufuateni nitakuwa nimekengeuka kuiacha Haki, na sitokuwa katika waongofu!
Waambie: Mimi nipo juu ya Sharia iliyo wazi, iliyo teremshwa kutoka kwa Mola wangu Mlezi. Na nyinyi mmeikanusha Qur'ani iliyo ileta Sharia hii. Na mimi sina uwezo kuileta hiyo adhabu mnayo ihimiza ije. Bali hayo yamo katika uwezo wa Mwenyezi Mungu, na yamelazimika na kupenda kwake na hikima yake. Na hakuna amri wala madaraka ila ya Mwenyezi Mungu tu. Akipenda Yeye atakuleteeni adhabu kwa haraka, na akipenda ataichelewesha. Yeye Subhanahu, Aliye takasika, anafuata katika hayo hikima yake, naye ni mbora wa kuhukumu baina yangu na nyinyi.
Sema: Lau ingeli kuwa kumo katika makadara yangu kukuteremshieni hiyo adhabu mnayo ihimiza ije, ningeli kuteremshieni kwa kukasirika kwa ajili ya Mola Mlezi wangu. Na hapo mambo yangeli kwisha baina yangu na nyinyi. Walakini amri ni ya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kujua kuliko wote wanayo stahiki makafiri katika adhabu ya haraka, au ya kuakhirika.
Ni Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ujuzi wa milango yote ya vilio ghaibu, visio juulikana na wengine. Hapana Mwenye kukusanya ujuzi wa hivyo ila Yeye, na anao wataka kuwapa baadhi yake. Naye ujuzi wake umekusanya vitu vyote vilioko nchi kavu na vilioko baharini. Wala halidondoki jani, jani lolote lile, ila Yeye analijua, wala haianguki mbegu chini ya ardhi, wala chochote kilicho kinyevu au kikavu, ila Yeye Subhanahu anakijua kwa utimilifu. Kauli hii inafahamisha kuwa kujua mambo ya ghaibu kuko kwa Mwenyezi Mungu, na funguo za hayo ziko kwake tu. Na mambo ya ghaibu ni mafungu mawili: Ghaibu Mut'laq ambayo hayumkini kutambulikana na akili, kama mambo yatakayo mfikia mtu katika mustakbali. Na Ghaib Nisbiy hizi ni siri za ulimwengu na viliomo ndani yake, na kuweza kuvitumia kwa maslaha ya watu. Ujuzi wa hayo huweza kughibu kwa vizazi kadhaa, kisha ukadhihiri.. Na funguo ya hizi pia ziko kwa Mwenyezi Mungu, humwezesha amtakaye katika waja wake wale wanao zama kuusoma ulimwengu. Na katika hayo ni haya ya uvumbuzi ambao tunauona anao ufikilia mwanaadamu kwa kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.