Na hayo masanamu wanayo yaomba kwa woga na kutafuta amani badala ya Mwenyezi Mungu pekee hayawajibu wito na maombi yao. Hali yao ni kama mwenye kukunjua kiganja chake akinge maji ya kunywa na kiganja kisifike mdomoni. Na hali yao ikiwa ni hii, basi hizo dua zao haziwi ila kupotea na kukhasirika.
Na vyote viliomo mbinguni na duniani, vitu, watu, majini, na Malaika, vinamnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa matakwa yake na utukufu wake, vikitaka visitake. Hata vivuli vyao kadhaalika, vikirefuka na kufupika kwa mujibu wa nyakati za mchana adhuhuri na jioni, kwa kufuata anavyo amrisha Mwenyezi Mungu na anavyo kataza.
Mwenyezi Mungu amemuamrisha Nabii wake ajadiliane na washirikina kwa kuwaongoa na kuwabainishia. Akamwambia: Ewe Nabii! Waambie: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi, naye ndiye Mwenye kuzilinda, na Mwenye kuviendesha viliomo humo? Tena uwaeleze jawabu iliyo sawa hiyo wanayo ishindania. Waambie: Huyo ni Mwenyezi Mungu anaye abudiwa kwa haki, hana mwenginewe. Basi ni waajibu wenu mumuabudu Yeye peke yake. Tena waambie: Mnaziona dalili zilizo thibiti zinazo onyesha uumbaji wake kila kitu peke yake? Na juu ya hivyo mnawafanya masanamu kuwa ni miungu, bila ya kukubali kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja! Na haya masanamu hayajifai wenyewe kheri wala shari! Vipi basi mnayafanya sawa na Muumba Mwenye kupanga? Nyinyi mnafanya sawa baina ya Muumba wa kila kitu na asiye miliki kitu! Mmekuwa kama anaye fanya sawa baina ya viwili vinavyo gongana! Basi hebu ni sawa baina ya mwenye kuona na asiye ona? Je, giza totoro na mwangaza unao ng'aa ni sawa? Je, usawa huo unaingia akilini mwao? Au upotovu wao umepita hadi hata wanadai kuwa hayo masanamu yao ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba na kupanga, hata yakawadanganyikia wasijue mambo ya uumbaji, kama walivyo potea katika kuabudu? Waambie ewe Nabii! Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Muumba wa kila kiliopo. Na Yeye ni peke yake katika kuumba na kuabudiwa, Mwenye kushinda kila kitu.
Na hakika neema zake Mtukufu mnaziona, na masanamu yenu hayana athari yoyote katika neema hizo. Yeye ndiye anaye kuteremshieni mvua kutoka kwenye mawingu, na mito na mabonde yakamiminika maji, kila kitu kwa kadiri yake aliyo ikadiria Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa ajili ya kuzalisha mimea, na matunda ya miti. Na mito inapo miminika hubeba juu yake visio kuwa na manufaa, na huwa katika hivyo vyenye nafuu hubakia, na visio na faida hupita. Mfano wa hayo ni Haki na baat'ili, kweli na uwongo. Haki hubakia na baat'ili ikapita. Na katika maadeni yanayo yayushwa kwa moto kwa kufanyia mapambo, kama dhahabu na fedha, na yanayo tumiwa kwa manufaa mengine kama chuma na shaba, kadhaalika sehemu isiyo na faida huwa juu kama povu na hutupwa. Na yenye nafuu ndio hubakia. Kadhaalika katika imani. Potovu hupita, na iliyo ya kweli hubakia. Kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu Subhanahu anabainisha ukweli wa mambo, na hupiganisha mifano hii kwa hii ili yote yabainike wazi.
Watu kwa mujibu wa kupokea kwao uwongofu ni mafungu mawili. Fungu moja lilio itikia wito wa Mwenyezi Mungu Muumba Mwenye kupanga. Hilo litapata malipo mema duniani na Akhera. Fungu jengine lisilo itikia wito wa Aliye waumba. Hawa watapata malipo maovu Akhera. Na lau kuwa wanamiliki kila kiliomo duniani na mfano wake mara ya pili, hawawezi kujikinga na hayo malipo maovu! Lakini watapata kumiliki hayo? Kwa hivyo yao wao ni hisabu ya kuwaudhi, na wataishia katika Jahannamu, na huko ni pahali paovu mno pa kuishi.