Alif Lam Mym 'Saad. (A.L.M.S'.) Hizi ni harufi za kutamkwa ambazo zinaanzia baadhi ya Sura za Makka, kwa ajili ya kuwazindua Washirikina kuwa hakika hii Qur'ani Tukufu imeundwa kwa harufi zile zile wanazo zitamka wao. Na juu ya hivyo wao wanaemewa hawawezi kuleta mfano wake. Kadhaalika harufi hizi zinapo somwa huwazindua wao wasikilize, kwa kuwa walikuwa wananasihiwa na wakubwa zao kuwa wasiisikilize Qur'ani.
(Ewe Nabii!) Umeteremshiwa wewe Qur'ani ili uwaonye hao wanao kanya wapate kuamini, na uwakumbushe Waumini wapate kuzidi Imani yao. Basi usiingie dhiki katika kifua chako unapo ifikilisha kwa kukhofu kuwa utakanushwa.
(Enyi Watu!) Fuateni aliyo kufunulieni Mola wenu Mlezi, wala msiwafuate marafiki au walinzi wengineo badala yake Yeye, mkawa mnawaitikia wao na mkiwaomba msaada! Itakuwa kama hamkuwaidhika ikiwa mtaiacha Dini ya Mwenyezi Mungu na muifuate nyengineyo, hali ya kuwa yapo mengi ya kuzingatia katika haya mliyo funuliwa.
Kwani Sisi tumekwisha iteketeza miji kadhaa wa kadhaa, kwa sababu watu wao walikuwa wakiwaabudu wasio kuwa Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa katika mwendo wao hawakufuata Njia yake. Ikawajia adhabu yetu wakati wao wameghafilika na wametuwa usiku nao wamelala, kama yalivyo wapata kaumu ya Lut'; au wakatekezwa mchana nao wamepumzika wakati wa kujinyoosha, kama yalivyo wapata kaumu ya Shua'ib.
Basi wakaungama kwa madhambi yao yaliyo waletea msiba wao. Hakuwa hata mmoja katika wao walipo ona adhabu ila alisema, na wakati huo kusema huko hakufai kitu: Hakika sisi tulikuwa tumejidhulumu nafsi zetu kwa maasiya, wala Mwenyezi Mungu hakutudhulumu kwa kutupa adhabu.
Na Siku ya Kiyama hisabu ya Mwenyezi Mungu itachungua kila kitu kwa uadilifu. Tutawauliza watu tulio watumia Mitume: Je, Ujumbe umewafikilia? Na wamewajibu nini hao Wajumbe tulio watuma? Na tutawauliza Mitume pia: Je, mmefikisha yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi? Na hao kaumu zenu wamekujibuni nini?
Na tutawapa wote khabari ya kweli yote yaliyo kuwa kwao, kwa sababu hakika Sisi tumewadhibitia kila kitu chao, kwani Sisi hatukuwa mbali nao, wala hatukuwa hatujui waliyo kuwa wakiyafanya.
Na Siku tutapo wauliza na kuwaeleza, vipimo vya vitendo vyao kwa ajili ya kulipwa vitakuwa vipimo vya uadilifu. Wale ambao mema yao yatazidi kuliko maovu yao watakuwa ndio wenye kufuzu, tutakao walinda na Moto na tutawatia Peponi.
Na wale ambao maovu yao yatakithiri kuliko mema yao, hao ndio watakuwa khasarani, kwa kuwa wameziuza nafsi zao kwa Shetani, wakaacha kuzingatia Ishara zetu kwa ukafiri na inda.
Nasi tumekuwekeni katika ardhi, na tukakupeni nguvu za kuiamirisha mkajipatia manufaa ndani yake, na tukakusahilishieni njia za kupatia maisha. Juu ya neema hizi zote, kumekuwa kuchache mno kumshukuru kwenu Mwenyezi Mungu. Nanyi mtakuja pata malipo ya hayo myatendayo!
Na katika khabari za wale wa mwanzo pana mazingatio na mawaidha, yanayo dhihirisha kuwa Shetani anajaribu akuondoleeni neema kwa kusahau kwenu amri za Mwenyezi Mungu. Sisi tumemuumba baba yenu Adam, na tukampa sura. Kisha tukawaambia Malaika: Mtukuzeni! Wakamtukuza kwa kut'ii amri ya Mola wao Mlezi, ila Iblisi hakut'ii.