Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Msiwafanye maadui wangu na maadui wenu kuwa ni wenzenu mkiwapa mapenzi ya kweli, na hali wao wameyakataa yaliyo kujieni nyinyi ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu chake. Wamemtoa Mtume na wamekutoeni nyinyi kwenu kwenye majumba yenu, kwa sababu ya Imani yenu kumuamini Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Mnapotoka makwenu kwenda pigana Jihadi katika Njia yangu na kutaka radhi yangu, basi msifanye urafiki na adui zangu, mkawapa mapenzi kisirisiri. Na Mimi nayajua vyema yote mnayo yaficha na mnayo dhihirisha. Na yeyote mwenye kumfanya adui wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiye rafiki yake basi ameikosea Njia Iliyo Nyooka.
Wakikutana nanyi na wakakuwezeni, uadui wao kwenu unadhihiri, na wanakunyoosheeni mikono yao na ndimi zao kukudhuruni. Na wanatamani muwe makafiri kama wao.
Hawatakufaeni kitu jamaa zenu wala watoto wenu mlio wafanya kuwa ni marafiki, na hali wao ni adui wa Mwenyezi Mungu na adui zenu. Katika Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atakutengeni mbali mbali. Atawatia maadui zake Motoni na marafiki zake Peponi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote myatendayo.
Nyinyi mna kiigizo kizuri cha kukiiga katika Ibrahim na walio amini pamoja naye, pale walipo waambia watu wao: Hakika sisi tunajitenga nanyi, na tunajitenga na hiyo miungu ya uwongo mnayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Sisi tunakukataeni, na umekwisha dhihiri uadui na kuchukiana baina yetu na nyinyi. Hayo hayataondoka kabisa mpaka mumuamini Mwenyezi Mungu peke yake. Lakini kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Nitakutakia maghfira, na similiki kwa Mwenyezi Mungu kitu chochote - kauli hiyo si ya kufuatwa. Kwani hayo yalikuwa kabla hajajua huyo baba yake kashikilia kuwa adui wa Mwenyezi Mungu wala hageuki. Ilipo dhihiri kwake kuwa hakika huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu alijitenga naye. Enyi waumini! Semeni: Mola wetu Mlezi! Kwako Wewe ndio tunategemea, na kwako Wewe tunarejea, na kwako Wewe ndio mwisho wetu Akhera.
Mola wetu Mlezi! Usitujaalie tukawa katika hali ya kuwa katika fitina za walio kufuru. Na tusamehe madhambi yetu, ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu usiye shindika, Mwenye hikima katika kutasarafu kwake.