Na akatimiza kuumba mbingu saba mnamo siku mbili nyengine. Na akaweka katika kila mbingu alicho kiandalia na ilivyo pelekea hikima yake. Na akaipamba mbingu ya karibu na dunia kwa nyota zinazo ng'ara kama taa, kwa ajili ya uwongofu wasisikilize mashetani khabari za walio juu. Kuumba huko vilivyo ni mpango wa Mwenyezi Mungu asiye shindika, Mwenye kuzunguka kila kitu.
Basi washirikina wakipuuza Imani baada ya kuwekewa wazi dalili zake, wewe, Mtume, waambie: Nimekuonyeni msije kupatilizwa kwa adhabu kali kama iliyo wateketeza kina A'di na Thamudi.
Walijiwa A'di na Thamudi na hiyo adhabu walipo watokelea Mitume pande zote. Hawakuacha njia ya kuwaongoza ila waliipitia, na wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Wao wakasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli taka kumtuma Mtume basi angeli tuteremshia Malaika. Basi sisi hakika tunakataa hayo ya Tawhidi na mengineyo mliyo kuja nayo nyinyi.
Ama kina A'di walipandwa na kiburi katika nchi bila ya haki ya kuwa na kiburi hicho. Na walisema kwa kughurika na nafsi zao: Nani huyo anaye tushinda sisi kwa nguvu? Ama ajabu watu hawa! Wanasema hayo na wao hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ana nguvu zaidi kuwashinda wao? Na wao walikuwa wakizikanya Ishara zetu!
Tukawapelekea upepo wenye sauti kali katika siku korofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwafanya wawe madhalili wanyonge katika maisha ya duniani. Na ninaapa kuwa bila ya shaka adhabu ya Akhera itakuwa ya hizaya zaidi, wala wao siku hiyo hawatapata wa kuwasaidia.
Na ama kina Thamudi tuliwabainishia njia ya kheri na njia ya shari. Lakini wao walikhiari upotovu kuliko uwongofu, ikawatwaa radi iliyo waunguza kwa madhila na unyonge, kwa sababu ya madhambi waliyo yachuma.
Ewe Nabii! Siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kupelekwa Motoni, wakawa wa mwanzo wao wanakutana na wa mwisho wao, ili ipate hoja ilazimike juu ya wote,
Mpaka watakapo ufikilia Moto na wakaulizwa juu ya madhambi waliyo yatenda duniani, na wao wakakataa, yakawashuhudilia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa waliyo yatenda wao,