Miongoni mwa Mayahudi kipo kikundi kazi yao kugeuza geuza maana ya maneno. Wao husema kimoyomoyo kumwambia Mtume s.a.w.: Tumesikia hayo maneno, na hatuifati hiyo amri. Na pia husema: Sikia maneno yetu - hukusikia wito. Wakikusudia kwa hayo kumuapiza Mtume. Na husema: Sikia bila ya kusikilizwa. Tamko hilo wanalipindua maana. Muradi wao ni kumuapiza, na wanajidai kuwa muradi wao ni kumwombea dua. Na husema: "Raai'na", wakipindua ndimi zao wakijitia kuwa wanakusudia "Undhurna" yaani "Tuangalie". Wanaonyesha kuwa wanataka uangalizi wake, na kumbe wanakusudia neno la Kiyahudi lenye maana ya "Mpumbavu" ili kuibeza Dini ya Kiislamu. Na lau kuwa wangeli nyooka sawa wakasema: "Tumesikia na tumet'ii" badala ya hiyo kauli yao ya "Tumesikia na tumeasi", na wakasema: "Sikia" na wasiseme "Bila ya kusikilizwa", na wakasema :"Undhurna" yaani "Tuangalie", badala ya "Raa'ina", ingeli kuwa bora kwao kuliko hayo wayasemayo, na ingeli kuwa ndiyo njia ya uadilifu zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewatoa katika rehema yake kwa ule upinzani wao. Kwa hivyo huwaoni miongoni mwao wanao mwitikia mwenye kuwaitia Imani ila wachache tu.