Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na kutokana na nafsi hiyo akamuumba mkewe, na kutokana na hao wawili, wakaenea wanaume na wanawake wengi. Basi nyote mnatokana na nafsi moja. Mcheni Mwenyezi Mungu mnaye mtaka msaada kwa kila mnacho kihitajia, na kwa jina lake ndio mnaombana nyinyi kwa nyinyi katika mambo yenu. Pia tahadharini na kuacha kuwasaidia jamaa zenu, wa karibu na wa mbali. Kwani Mwenyezi Mungu daima anakuangalieni. Hapana chochote katika mambo yenu kinacho fichikana kwake. Na Yeye ndiye Mwenye kukulipeni.