Huu ni uteremsho wa Qur'ani umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Na Yeye ndiye mwenye kupanga mambo yao. Hapana shaka yoyote kuwa hii imeteremka kutoka kwake.
Ati wanasema: Kaizua Muhammad, naye akamsingizia Mwenyezi Mungu! Haiwafalii wao kusema hayo. Kwani hii ni Haki, Kweli, iliyo teremka kutokana na Mola wako Mlezi, ili upate kuwakhofisha kwayo watu ambao hawajapata kujiwa na Mtume kabla yako, utaraji kwa onyo hili wapate kuongoka na waifuate Haki.
Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi na vilio baina yao kwa siku sita, kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi, A'rshi, kwa utawala ulio laiki naye. Nyinyi hamna badala yake Yeye yeyote msaidizi wa kukunusuruni, wala mwombezi wa kukuombeeni. Basi je, mtaendelea kushikilia kuwa katika ukafiri na inda, wala msiwaidhike kwa mawaidha ya Mwenyezi Mungu?
Yeye huyaendesha mambo ya uumbaji katika mbingu na ardhi, kisha amri yake hupanda kwenda kwake kwa siku ambayo kadiri yake ni kama miaka elfu kwa mujibu wa miaka ya duniani mnayo ihisabu nyinyi.
Huyo ndiye aliye sifika kwa kuumba na kutawala na kupanga, Mwenye kuyajua ya ghaibu ya viumbe vyote na wanayo yaona, ambaye amri yake ni yenye kushinda, Mkunjufu wa rehema,
Aliye umba kila kitu kwa ustadi, kwa mujibu wa inavyo hitajia hikima yake, na akaanza kumuumba mtu wa mwanzo kwa udongo,
Kisha akawafanya dhuriya zake wa namna mbali mbali kutokana na maji machache, dhaifu, yasiyo tamanika kwa kawaida. Katika Aya hii tukufu "utokane na kizazi cha maji dhaifu". Neno la Kiarabu lilio tumiwa ni "Mahiin". Neno hili likitumiwa kwa mtu lina maana ya "dhaif", mnyonge, na pia lina maana ya "chache". Basi kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Min maain mahiin" maana yake ni "kutokana na maji machache dhaifu" , ndiyo ya kudharauliwa. Mfano wa hayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Au mimi si bora kuliko huyu aliye (mahiin) mnyonge wala hawezi kusema waziwazi?" (Azzukhruf: 43.52). Na neno "Mahana al-ibila" maana yake "Kamkama maziwa ngamia". Kwa hivyo basi hapana ubaya kulifasiri neno hili Mahiin katika Aya hii kwa maana ya maji yanayo toka kwa kuchupa, au kumiminika, (kama yanavyo toka maziwa kwenye chuchu) au machache.
Kisha akamsimamisha na kumkuza, na akamtia ndani yake siri yake aliyo mkhusisha nayo, na akakupeni masikio, na macho, na akili, mpate kusikia na kuona na kufahamu. Nanyi hamshukuru ila kwa uchache.
Na wanao kanya kufufuliwa wakasema: Ati sisi tukisha kuwa mchanga, ulio changanyika na mchanga wa ardhi, usibagulike, ndio kweli tutarejea kwa umbo jipya? Hao hakika si kama wanakanya kufufuliwa tu, bali wanakadhibisha yote yatayo kuwako Akhera.
Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti, aliyewakilishwa kuzikamata roho zenu utapo kwisha muda wenu. Kisha kwa Mwenyezi Mungu peke yake ndio mtarejea.