Sema, ewe Nabii! Enyi Watu wa Kitabu! (Biblia, yaani Mayahudi na Wakristo) njooni kwenye neno moja la uadilifu lenye kutukusanya sote na tunalo litaja, nalo ni kuwa hatumuabudu ila Mwenyezi Mungu tu, wala tusimwekee washirika katika ibada. Na wala tusiwe tunawat'ii baadhi yetu tukiwafuata katika kuhalalisha na kuharimisha, tukaachilia mbali hukumu ya Mwenyezi Mungu katika mambo ya halali na haramu. Wakiukataa wito huu wa haki waambie: Shuhudieni kuwa sisi ni Waislamu, yaani tunafuata hukumu za Mwenyezi Mungu, na Yeye tu tumemsafia Dini, wala hatumwombi mwengineyo. (Taurati:Kutoka 20.3:Usiwe na miungu mingine ila Mimi. Injili ya Marko 12.29 : Yesu akamjibu, [amri] Ya kwanza ndiyo hii, Sikia Israel, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja.)