Kisha Mwenyezi Mungu baada ya dhiki akakupeni neema ya utulivu, ambao ulidhihiri kwa usingizi ulio wafunika wale walio wa kweli katika Imani yao na kumtegemea kwao Mwenyezi Mungu. Ama kile kikundi kingine, hamu yao ni juu ya nafsi zao tu hawana jenginelo; kwa hivyo wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbovu za kijahiliya, wakisema kwa kuchukiwa: Tumepata ushindi wowote sisi huo tulio ahidiwa? Sema ewe Nabii: Mambo yote ya kushinda na kushindwa yako kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kuyaendesha mambo kwa waja wake pindi wao wakichukua khatua za ushindi, au wakifanya mambo ya kusabibisha kushindwa. Na wao wanapo sema hayo wana jambo wanalo lificha katika nafsi zao, wala hawalidhihirishi. Kwani wao husema: Ingeli kuwa sisi tuna khiari yetu tusingeli toka, basi tusingeli shindwa. Waambie: Hata mngeli kuwa ndani ya majumba yenu na kama wapo walio andikiwa kuuliwa basi hapana shaka wangeli toka mpaka pahala pao pa kufa wakauliwa. Na Mwenyezi Mungu amefanya aliyo yafanya hapo Uhud kwa maslaha makubwa, ili apate kutoa ndani yenu ikhlasi, na azitahirishe nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua vilivyo yaliyo fichika ndani ya nyoyo zenu.