Siku mtapo kiona Kiyama mtaona kitisho chake kinafikilia ukubwa wake hata kama yupo mwanamke anaye nyonyesha na ziwa lake limo katika mdomo wa mwanawe, basi hapana shaka atamsahau na amwachilie mbali. Na kama yupo mwanamke ana mimba basi ataiharibu mimba kabla ya kufika wakati wake wa kuzaa kwa ajili ya fazaa na kitisho. Na ewe mwenye kuangalia! Ukiona hali ya watu Siku hiyo namna wanavyo onekana hawanazo, na wanapo kwenda wanayumba, utadhani wamelewa, na ilhali hawakulewa. Lakini kitisho walicho kishuhudia, na khofu ya adhabu kuu ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyo waondoshea utulivu wao.