Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni usiku wa kufunga kuingiana na wake zenu, na wao kuchanganyika nanyi katika maisha na katika malazi. Ilikuwa ni mazito kwenu kujitenga nao, na sasa mmepunguziwa hizo taabu. Mwenyezi Mungu anajua kuwa mlikuwa mkijipunguzia starehe ya nafsi zenu na mkijidhulumu kwa kujizuia msiingiane na wake zenu hata usiku wa Ramadhani. Sasa amekusameheni na kukupunguzieni mikazo. Sasa basi msione vibaya kuchanganyika nao, na stareheni kwa aliyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, na kuleni na mnywe usiku wa Ramadhani mpaka mwone mwangaza wa alfajiri unapo tokeza kutokana na kiza cha usiku. Hapo tena fungeni na mtimize Saumu mpaka linapo kuchwa jua. Na ilivyo kuwa Saumu ni katika ibada zinazo taka mtu kujiepusha na matamanio ya roho na kuingiana na wanawake wakati wa mchana, basi kadhaalika katika ibada ya kukaa Itikafu msikitini inahitaji kujitenga na kuacha kustarehe na wake zenu wakati huo mnapo kuwapo katika Itikafu. Na haya ya sharia za Saumu na Itikafu alizo kuwekeeni Mwenyezi Mungu yashikeni baraabara msikaribie kuyavunja. Na Mwenyezi Mungu ameyaweka wazi haya kwa watu kwa namna hii ili wapate kuyaogopa na waepukane na matokeo yake.