Na kumbukeni enyi Wana wa Israili! Tulipo kwambieni: Ingieni katika mji mkubwa aliyo kutajieni Nabii wenu Musa na mle katika viliomo humo kama mnacho kitaka, kwa wingi na kwa wasaa, kwa sharti lakini kuwe kuingia kwenu kwa upole na unyenyekevu, kupitia mlango aliyo utaja Nabii wenu. Na kwamba hapo mumuombe Mwenyezi Mungu akusameheni makosa yenu. Kwani mwenye kufanya hayo kwa ikhlasi, usafi wa niya, tunamfutia makosa yake. Na mwenye kuwa mtenda mema aliye mt'iifu tunamzidishia thawabu na ukarimu juu ya kumsamehe na kumfutia dhambi.
Lakini walio dhulumu walikwenda kinyume na amri za Mola wao Mlezi, wakasema sio walio amrishwa wayaseme, kwa kudhihaki na kuasi. Basi jaza yao ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwateremshia juu yao adhabu kuwa ndiyo malipo ya ukosefu wao na kuzivunja amri za Mola wao Mlezi.
Na kumbukeni, enyi Wana wa Israili, siku Nabii wenu Musa alipo taka maji kutokana na Mola wake Mlezi kiliposhtadi kiu jangwani, Nasi tukakurehemuni. Tukamwambia Musa: Lipige jiwe kwa fimbo yako, yakatimbuka maji kutoka chemchem kumi na mbili. Kila kikundi na chemchem yake, na walikuwa makundi thinaashara Kumi na mbili. Basi kila kabila ikawa na pahala pake pa kunywea. Na tukakwambieni: Kuleni Manna na Salwa, na kunyweni maji haya yanayo timbuka, na muwache mlio nayo, wala msipite mipaka kwa uharibifu katika nchi, bali wacheni maasia.
Na kumbukeni pia, enyi Mayahudi, pale wale wazee wenu walio tangulia walipo zidi jeuri zao, wasiipe neema ya Mwenyezi Mungu haki yake, wakamwambia Musa: Sisi hatutovumilia chakula hicho kwa hicho (nacho ni Manna na Salwa). Basi muombe Mola wako atutolee katika ardhi mboga, na matango, na adasi, na thom na vitunguu. Musa aliyastaajabia haya na wala hakupendezewa nayo. Akawaambia: Hivyo nyinyi mnafadhilisha vyakula namna hii kuliko vilivyo kuwa bora zaidi na vizuri zaidi, navyo ni Manna na Salwa? Basi shukeni kutoka Sinai, na ingieni katika mji mmojawapo na huko mtapata hivyo mnavyo vitaka. Na kwa sababu ya kutoridhika kwao huko na inda yao hao Mayahudi walipigwa na madhila, na ufakiri na unyonge, wakastahiki kupata ghadhabu ya Mwenyezi kwa ule mtindo wao wa inda na uasi, kukanusha ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa Manabii. Kwa haya ikawa wanaacha Haki iliyo kwisha thibiti na kukubalika. Yaliyo wapelekea hata wakaingia katika ukafiri ule na mauwaji yale ni kule kuziachia nafsi zao kupanda maasi na kufanya uadui na kupindukia mipaka katika maasia.