Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako, ewe Nabii, ila kwa lugha ya kaumu yake ile tuliyo mtumia, ili apate kuwafahamisha aliyo kuja nayo, na wao wayafahamu, na wayaelewe kwa wepesi. Wala si juu yake yeye kuwa lazima waongoke. Mwenyezi Mungu Mwenyewe ndiye humwacha apotee anaye mtaka kwa kuwa huyo si tayari kuitaka Haki. Na humwongoa amtakaye kwa kuwa kajitayarisha vyema kufuata Haki. Naye Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu ambaye hashindiki kwa atakalo, na ambaye anayapanga mambo yote kwa mahala pao. Basi haachi kupotea wala haongoi ila kwa hikima yake.