Na Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, ndiye aliye kukunjulieni ardhi, akaidhalilisha ili muweze kutembea juu yake mashariki na magharibi. Na Yeye akajaalia katika hii ardhi milima iliyo simama imara, na mito ya maji matamu inayo miminika. Na akajaalia kwa hayo maji matunda ya kabila mbali mbali yanayo zaliana, na kati ya kabila hizo namna mbali mbali, mengine matamu na mengine makali, mengine meupe, na mengine meusi. Na Yeye Subhanahu huufunika mchana kwa usiku. Na hakika katika huu ulimwengu na ajabu zake zimo alama wazi za kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na Umoja wake kwa anaye fikiri akazingatia. Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia katika kila mimea dume na jike ili ipate kupandishika sehemu ya uke kwa chembe za uzazi zilioko katika sehemu za ume. Na kwa hivyo ndio huzalikana namna kwa namna na kwa wingi.