Na hakika neema zake Mtukufu mnaziona, na masanamu yenu hayana athari yoyote katika neema hizo. Yeye ndiye anaye kuteremshieni mvua kutoka kwenye mawingu, na mito na mabonde yakamiminika maji, kila kitu kwa kadiri yake aliyo ikadiria Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa ajili ya kuzalisha mimea, na matunda ya miti. Na mito inapo miminika hubeba juu yake visio kuwa na manufaa, na huwa katika hivyo vyenye nafuu hubakia, na visio na faida hupita. Mfano wa hayo ni Haki na baat'ili, kweli na uwongo. Haki hubakia na baat'ili ikapita. Na katika maadeni yanayo yayushwa kwa moto kwa kufanyia mapambo, kama dhahabu na fedha, na yanayo tumiwa kwa manufaa mengine kama chuma na shaba, kadhaalika sehemu isiyo na faida huwa juu kama povu na hutupwa. Na yenye nafuu ndio hubakia. Kadhaalika katika imani. Potovu hupita, na iliyo ya kweli hubakia. Kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu Subhanahu anabainisha ukweli wa mambo, na hupiganisha mifano hii kwa hii ili yote yabainike wazi.