Na yule bibi aliye kuwa Yusuf anakaa nyumbani kwake, naye anamjua madaraka yake, alitaka kumghuri aache mwendo wake ulio safi. Akawa anajipitisha pitisha mbele yake kuonyesha uzuri wake, na kujitamanisha kwake. Hata mwishoe akamfungia milango, na akamwambia: Njoo kwangu, nimejitoa kwako! Yusuf akasema: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu, aniepusha na hiyo shari! Na vipi nifanye uchafu huo nawe, na mumeo mheshimiwa ni bwana wangu aliye niweka bora ya makamo? Hakika hawafuzu wanao wadhulumu watu kwa udanganyifu na khiana, wakajitia wenyewe katika maasi ya uzinzi!