Yusuf akamwelekea Mwenyezi Mungu akimshukuru kwa kuzihisabu neema zake juu yake, na akimwomba amzidishie fadhila zake, kwa kusema: Ewe Mola wangu Mlezi! Neema zako kwangu ni nyingi mno, na bora mno! Umenipa utawala, na nakuhimidi kwa hayo. Ukanitunukia ilimu ya kufasiri ndoto kama ulivyo nitunukia! Ewe Muumba mbingu na ardhi! Wewe ndiye uliye miliki mambo yangu yote, na Mtawala wa neema za uhai wangu na baada ya kufa kwangu! Nifungamanishe nawe kwa ulivyo waridhia Manabii wako katika Dini ya Kiislamu, na uniingize katika kundi la ulio waongoa kwenye wema miongoni mwa baba zangu, na waja wako walio wema, walio safika.