Enyi Waumini, piganeni nao! Mwenyezi Mungu atawaonjesha adhabu itokayo mikononi mwenu, na atawadhalilisha na atakupeni ushindi juu yao. Na kwa kuwashinda hao, na kuunyanyua utukufu wa Uislamu, Mwenyezi Mungu atayapoza machungu yaliyomo katika vifua vya Waumini, yaliyo fichikana na yaliyo dhihiri, wakati wote walipo kuwa wakipata maudhi ya makafiri.
Na Mwenyezi Mungu atazijaza nyoyo za Waumini furaha ya kushinda baada ya kuwa na hamu na khofu, na atawaondolea hasira, na Mwenyezi Mungu atapokea toba ya amtakaye kumkubalia katika wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa ujuzi kwa mambo yote ya waja wake, ni Mkuu wa hikima katika anayo waamrisha.
Enyi Waumini! Msidhani kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuacheni hivi hivi bila ya kukutieni mtihanini kwa Jihadi na mfano wa hayo. Ndio mwendo wake Mwenyezi Mungu kufanya mitihani, upate dhihiri ujuzi wake kwa wale kati yenu wanao pigana Jihadi, wenye ikhlasi (yaani nyoyo safi), na wala hawawafanyi marafiki, wendani na walinzi, isipo kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wenzao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema vitendo vyenu vyote, na atakulipeni kwavyo.
Hawawi washirikina ndio wenye kufaa kuamirisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu, na hali wao wangali kuendelea na ukafiri wao, na wanautangaza khasa! Vitendo vyao washirikina havitiwi hisabuni, wala hawatolipwa thawabu kwavyo! Wao ni wenye kudumu Motoni Siku ya Kiyama.
Lakini wanao amirisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja peke yake, na wakasadiki kuwapo kufufuliwa na kulipwa, na wakatimiza Swala kama itakikanavyo, na wakatoa Zaka ya mali yao, na wala hawamwogopi ila Mwenyezi Mungu peke yake. Na hao ndio wanao tarajiwa kuwa mbele ya Mwenyezi Mungu waongofu wa kufuata Njia Iliyo Nyooka.
Haifalii kuwafanya washirikina wanao wanywesha maji Mahujaji, na wakauamirisha Msikiti Mtakatifu (wa Makka), katika cheo kama cha wanao muamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na wakasadiki kufufuliwa na kulipwa kwa wayatendayo, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu..Hao si makamu mamoja mbele ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kwenye Njia ya kheri watu ambao wameshikilia kujidhulumu wenyewe kwa ukafiri wao, na wakawadhulumu wengineo kwa maudhi yasio kwisha.
Wale walio sadiki kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja, na wakauhama mji wa ukafiri kuendea mji wa Uislamu, na wakavumilia mashaka ya Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa kutoa mali yao na roho zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, kuliko wengineo wasio na sifa hizi. Na hawa ndio wenye kufuzu, kuzipata thawabu za Mwenyezi Mungu na ukarimu wake.