Hakika kimempitia mwanaadamu kipindi cha zama kabla hajapuliziwa roho, naye hata bado hakuwa ni kitu cha kutajika kwa jina lake, wala hajuulikani nini atakuwa.
Hakika Sisi tumemuumba mwanaadamu naye ana sifa namna mbali mbali, kwa ajili ya kumtia mtihanini, majaribioni, baadaye. Kwa hivyo tukamjaalia awe anasikia na anaona, ili apate kuzisikia Aya na azione Ishara.
Na huwalisha chakula mafakiri wasio weza kazi, na watoto walio fiwa na wazee wao, na wafungwa wasio miliki kitu, ijapo kuwa wao wenyewe hao watoaji wanakipenda hicho wanacho kitoa, na wanakihitajia.
Na hujiambia nafsi zao: Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutaka thawa;bu za Mwenyezi Mungu. Sisi hatutaki kwenu malipo au zawadi, wala hatutaki kushukuriwa na kusifiwa.
Basi Mwenyezi Mungu akawalinda na shida za siku hiyo, na badala ya mkunjo wa wenye maasi, akawapa nyuso za kupendeza, na ukunjufu na furaha katika nyoyo zao,
Na watakuwa wanawazunguka vijana ambao hawabadiliki hali yao, kwa furaha na sururi. Ukiwaona wanapo zunguka kwa wepesi na uchangamfu, utawadhania kwa uzuri wao na usafi wa rangi zao, kama lulu zilizo tandazwa mbele yako zinang'ara.
Juu yao zipo nguo za hariri nyepesi za kijani, na nguo za hariri nzito. Na mapambo yao yaliomo mikononi mwao ni vikuku vya fedha. Na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji kingine kilio safi, hakina uchafu wala najisi.
Hakika neema hizi ameziandaa kwa kukulipeni kwa vitendo vyenu. Na hizo juhudi zenu duniani ni zenye kusifika kwa Mwenyezi Mungu, na zinampendeza, na zimekubaliwa.
Basi subiri, uivumilie hikima ya Mola wako Mlezi kwa kuakhirisha kushinda kwako kuwashinda maadui zako, na wewe ukapata mitihani kwa maudhi yao. Wala usiwat'ii washirikina, wingi wa madhambi, walio zama katika ukafiri.
Hakika hawa makafiri wanaipenda dunia, na wanaifadhilisha kuliko Akhera. Na wanaiacha migongoni mwao siku yenye misiba mikubwa, na vitisho vikali. Wala wao hawajui nini cha kuwaokoa wao na hayo!
Sisi tumewaumba wao, na tumefanya kwa hikima kuumbwa kwao. Na tukitaka tutawateketeza wao na tutawaleta mfano ya wao badala yao, ambao hao watakuja kumt'ii Mwenyezi Mungu kinyume na wao.
Hakika Sura hii ni mawaidha kwa walimwengu wote. Basi mwenye kutaka atafuata njia ya Imani na uchamngu kwendea kwa Mola wake Mlezi imfikishe kwenye maghfira yake na Pepo yake.
Wala nyinyi hamwezi kutaka kitu chochote ila wakati anapo taka Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zenu, Mwenye hikima kwa anayo yataka na akayakhiari.
Humuingiza amtakaye katika Pepo yake. Basi kuingia Peponi ni kwa fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu. Naye amewadhalilisha wenye kudhulumu, amewatengenezea adhabu iliyo chungu.