Hao wanaafiki wanaapa mbele yako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba hawakusema jambo baya katika hayo uliyo ambiwa. Nao ni waongo katika kukataa kwao, wanaapa kiapo cha uwongo! Na wao hakika wamesema neno la kufuru. Na ukafiri wao sasa umebainika, baada ya kuwa kwanza umefichika. Na hapana sababu yoyote ya kukuchukia ila ni kiburi kwa neema walizo pewa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa kule kupewa ngawira walizo shirikiana na Waislamu! Wakirejea kwa Mwenyezi Mungu, wakaacha unaafiki wao, na wakajuta kwa waliyo yatenda, toba yao itakubaliwa. Na hivyo itakuwa kheri kwao. Wakiitupa Imani, basi Mwenyezi Mungu atawaadhibu duniani kwa namna mbali mbali za balaa, na kesho Akhera atawatia katika Moto wa Jahannamu. Wala hawatapata katika ardhi wa kuwapigania, au wa kuwaombea, au wa kuwanusuru.