Itakuwaje hawa washirikina, wanao vunja ahadi mara kwa mara, wawe na ahadi ya kuhishimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake? Basi msichukue ahadi zao, ila wale katika kabila za Kiarabu mlio ahadiana nao kwenye Msikiti Mtakatifu, na kisha wakasimama sawa kwenye ahadi yao. Basi nanyi simameni sawa juu ya ahadi yenu maadamu wao wamesimama sawa. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye kumt'ii Yeye na wenye kutimiza ahadi zao.
Vipi nyinyi mtalinda ahadi zao nao ni watu ambao wakikuwezeni wanawasaidia maadui zenu dhidi yenu? Hawataacha fursa ya kukumalizeni bila ya kujali ujamaa (udugu) wala mapatano. Na watu hao hukudanganyeni kwa maneno yao yaliyo pakwa asali, na nyoyo zao zimekunja kwa kukuchukieni. Na wengi wao wametokana na Haki, ni wenye kuvunja ahadi.
Wamezitupa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakazibadilisha hizo kwa machache yasiyo dumu ya kidunia, na wakazuia watu wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu. Hakika wafanyayo watu hawa ni mabaya!
Hiyo ndiyo hali ya ukafiri wao. Hawahishimu ujamaa wala ahadi katika kuamiliana na Muumini. Shani ya watu kama hao ni kufanya uadui tu. Hayo ndiyo maradhi yao yasio wabanduka!
Wakitubia, wakaacha ukafiri wao, na wakashika hukumu za Uislamu, kwa kushika Swala, na kutoa Zaka, basi wanakuwa ni ndugu zenu katika Dini. Haki yao kama haki yenu. Jukumu lao kama jukumu lenu. Na Mwenyezi Mungu anazibainisha Aya hizi kwa watu wanao nafiika na ilimu.
Na pindi wakivunja ahadi zao baada ya kwisha zikubali, na wakaendelea kuitukana Dini yenu, basi wapigeni vita wakuu wa upotovu na walio pamoja nao, kwani hao hawana ahadi wala dhima, ili wapate kuacha ukafiri wao.
Enyi Waumini! Kwa nini msikimbilie kwenda vitani kuwapiga vita washirikina walio vunja mapatano yenu mara kwa mara, na wao walikuwa wakijihimu kumfukuza Mtume Makka na kumuuwa, na wao tena ndio walio kuanzeni kukuteseni na kukufanyieni uadui tangu mwanzo? Je, mnawaogopa? Msiwaogope! Mwenyezi Mungu tu peke yake ndiye anaye stahiki nyinyi mumwogope, kama nyinyi ni wakweli katika Imani yenu.