Tena Hud akawaambia: Hivyo mmestaajabu mno, na mkaona mageni kukujieni ukumbusho wa Haki kwa ulimi wa mtu aliye mmoja wenu, kukuonyeni? Mkiendelea na haya mliyo nayo matokeo yake yatakuwa ni mabaya mno. Na hakika jambo hilo si la kustaajabiwa. Kisha Huud akawatajia yaliyo wasibu walio kanusha katika watu walio watangulia, na akawakumbusha neema za Mwenyezi Mungu juu yao. Akasema: Kumbukeni Mwenyezi Mungu alivyo kufanyeni ndio warithi wa nchi baada ya kaumu ya Nuhu alio waangamiza kwa kumkadhibisha Nuhu, na Mwenyezi Mungu akakuzidishieni nyinyi nguvu za mwili na nguvu za utawala. Na neema hizo zinatakikana zilete Imani. Basi zikumbukeni neema zake ili mpate kufuzu.