Musa alipo timiza muda wake walio patana, na akawa mume wa binti wa yule aliye mpokea, na akawa anarudi Misri, aliona njiani mwake katika upande wa Mlima wa T'uri moto unawaka. Akawaambia walio kuwa pamoja naye: Kaeni hapa. Mimi nimeuona moto, nimefurahi nao katika giza hili. Nitawendea nikuleteeni khabari ya njia, au nipate kijinga cha moto mpate walau moto wa kuota kujilinda na baridi.
Musa alipo ufikia moto alio uona alisikia kutoka upande wa kulia kwenye mti wenye kumea katika eneo lilio barikiwa ubavuni mwa Mlima, wito wa juu ukisema: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana anaye stahiki kuabudiwa isipo kuwa Yeye, Mwenye kuumba viumbe vyote na ni Mwenye kuvilinda na kuvihifadhi na kuvilea.
Na akanadiwa: Tupa chini fimbo yako. Akaitupa chini. Mwenyezi Mungu akaigeuza ikawa nyoka. Musa alipo iona inakwenda kama nyoka alikhofu, na akakimbia kwa kufazaika. Akaambiwa: Ewe Musa! Njoo, unaitwa urejee pahala pako, wala usiogope. Kwani wewe ni katika walio hifadhiwa na kila cha kuchukiza.
Na uingize mkono wako kwenye uwazi wa nguo yako utatoka mweupe, bila ya ila wala maradhi. Na jiambatishe mkono wako ubavuni mwako katika nguo ukiwa una khofu. Wala usishituke kwa kuona fimbo imekuwa nyoka, na kuona mkono wako umekuwa mweupe. Kwani miujiza hii miwili inatokana na Mwenyezi Mungu ya kumkabili nayo Firauni na kaumu yake watapo ukabili Ujumbe wako kwa kuukadhibisha na hali wametoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
Musa akasema, kwa khofu na kuomba msaada: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimemuuwa mtu katika hao, na nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi.
Na ndugu yangu, Harun, ni fasihi zaidi ulimi wake kuliko mimi. Basi mtume awe pamoja nami katika kufikisha Utume, kwani mimi nina khofu watanikanusha.
Mwenyezi Mungu akasema, kuitikia ombi lake: Tutakutia nguvu kwa kumtuma Harun. Na tutakupeni nyinyi wawili madaraka, na tutakuungeni mkono kwa miujiza. Kwa hivyo hawatoweza kukuvamieni. Na nyinyi wawili na walio kufuateni na wakaongoka kwa msaada wenu, mtakuwa wenye kuwashinda hawa makafiri.