Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni usiku wa kufunga kuingiana na wake zenu, na wao kuchanganyika nanyi katika maisha na katika malazi. Ilikuwa ni mazito kwenu kujitenga nao, na sasa mmepunguziwa hizo taabu. Mwenyezi Mungu anajua kuwa mlikuwa mkijipunguzia starehe ya nafsi zenu na mkijidhulumu kwa kujizuia msiingiane na wake zenu hata usiku wa Ramadhani. Sasa amekusameheni na kukupunguzieni mikazo. Sasa basi msione vibaya kuchanganyika nao, na stareheni kwa aliyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, na kuleni na mnywe usiku wa Ramadhani mpaka mwone mwangaza wa alfajiri unapo tokeza kutokana na kiza cha usiku. Hapo tena fungeni na mtimize Saumu mpaka linapo kuchwa jua. Na ilivyo kuwa Saumu ni katika ibada zinazo taka mtu kujiepusha na matamanio ya roho na kuingiana na wanawake wakati wa mchana, basi kadhaalika katika ibada ya kukaa Itikafu msikitini inahitaji kujitenga na kuacha kustarehe na wake zenu wakati huo mnapo kuwapo katika Itikafu. Na haya ya sharia za Saumu na Itikafu alizo kuwekeeni Mwenyezi Mungu yashikeni baraabara msikaribie kuyavunja. Na Mwenyezi Mungu ameyaweka wazi haya kwa watu kwa namna hii ili wapate kuyaogopa na waepukane na matokeo yake.
Mmekatazwa siku zote kula mali ya watu kwa njia isiyo ya haki. Mali ya mtu si halali kwenu ila kwa moja ya njia alizo wekea Sharia Mwenyezi Mungu, kama vile mirathi, au kutunukiwa kwa kupewa na mwenye mali, au kwa mkataba ulio sahihi wenye kuhalalisha kumiliki. Na huenda mmoja wenu hutafuta njia za kumpokonya mwenziwe haki ya mali yake kwa kupeleka kesi mahkamani ili yeye kwa kushirikiana na mahakimu au makadhi na kuleta ushahidi wa uwongo, au uwongo dhaahiri, au kutoa rushwa, wapate kula mali kwa dhulma. Huo ni uovu mno kwa wanao tenda, na malipo yao ni mabaya sana.
Na watu wanakuuliza khabari za mwezi, unaanza mwezi mchanga kama uzi, kisha unakua mpaka unatimia kaamili. Tena unapungua mpaka unakuwa kama ulivyo anza. Haukai katika hali moja kama jua. Nini maana ya kugeuka huku hata inakuwa kila siku 29 au 30 unakuja mwezi mpya? Waambie: Huku kutokea hivi kuandama mwezi na kugeuka yapo ndani yake maslaha ya Dini na dunia pia. Hizi ni alama za kuonyesha nyakati za mambo ya maisha yenu. Zinaonyesha nyakati za Hija, ambayo ni moja katika Nguzo za Dini yenu. Na lau kuwa mwezi ungeli baki namna moja tu kama jua, msingeli tambua nyakati za maisha yenu na Hija zenu. Wala huko kutojua hikima ya kugeuka mwezi kusikupelekeeni kutilia shaka hikima ya Muumba. Wala sio wema kuziingilia nyumba kwa nyuma, kinyume na wafanyavyo watu wote. Lakini wema ni kumchamngu katika nyoyo na kumsafishia niya, na kuziingilia nyumba kwa kupitia milangoni kama wafanyavyo watu wote. Na mtake Haki na dalili iliyo sawa. Basi takeni radhi ya Mwenyezi Mungu, na muiogope adhabu yake na kwa hivyo ndio mtaraji kufanikiwa kwenu, na kufuzu kwenu na kuepuka adhabu ya Moto. Uislamu unahisabu mwezi unapo andama na kugeuka sura kwa watu kupimia nyakati za ibada, na pia kwa mambo yao ya kidunia, kwa sababu hayo ni mambo ya kuonekana, na kwa hivyo taarikhi inajuulikana kwa sura ya mwezi. Mwezi kwa hakika ni kama kioo kinacho onyesha mwangaza wa jua huku duniani. Mwezi ukiwa kati baina ya jua na dunia hauonekani, na baadae mwezi mchanga unaandama na wakaazi wa dunia wanajua kuwa mwezi mpya umeanza. Ukifika mwezi katika upande unao kabiliana baina ya jua na dunia ndio unapo kuwa wakati wa mbaamwezi, mwezi mpevu. Khalafu unaendelea kupungua kama ulivyo kuwa kwanza ukizidi kukua. Kwa hivyo taarikhi inaanza tangu pale ulipo kuwa mwezi mchanga. Pale unapo onekana mwezi mchanga kama uzi ndio mwezi umeandama, huonekana upande wa magharibi, hata kwa dakika chache baada ya kuchwa jua nao hupotea. Hivyo hivyo siku baada ya siku huhisabiwa mpaka zipite siku 29 au 30.
Na katika kumcha Mwenyezi Mungu ni kustahamili mashaka katika kumt'ii Yeye, na mashaka makubwa kabisa juu ya nafsi ni kuwapiga vita maadui wa Mwenyezi Mungu. Lakini wakikuvamieni, basi piganeni na hao wavamizi. Na mmepewa ruhusa kuurudi uvamizi wao, lakini nyinyi msivamie kwa kuanza nyinyi, au kwa kumuuwa asiye kupigeni vita wala hana mahusiano na vita; kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wavamizi.