Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio laiki naye. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda ambaye hashindwi na kitu. Mwenye hikima katika mipango yake na vitendo vyake.
Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banu Nnadhir, kutoka kwenye majumba yao wakati wa kuwatoa mara ya kwanza katika Bara Arabu. Enyi Waislamu! Hamkudhania kuwa watatoka kwenye nyumba zao kwa sababu ya nguvu zao. Na wao wenyewe walidhani kwamba ngome zao zitawalinda na mashambulio ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akawatokea katika upande wasio utarajia, na akawatia katika nyoyo zao fazaa kubwa, wakawa wanabomoa nyumba zao kwa mikono yao ili zibaki kuwa magofu tu, na kwa mikono ya Waumini wapate kuzivunja zile ngome. Basi enyi wenye akili, chukueni somo katika haya yaliyo washukia hawa.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwahukumia kuwatoa majumbani kwao kwa sura hii ya kuchusha, basi hapana shaka angeli waadhibu katika dunia kwa shida zaidi kuliko huko kuwatoa. Na Akhera, wao watapata adhabu ya Moto, mbali huku kutolewa majumbani kwao duniani.