Na wakikuona, ewe Nabii, wale walio mkataa Mwenyezi Mungu na ulio kuja nayo wewe, hawakufanyii wewe ila maskhara na kejeli. Huambiana wao kwa wao: Ndiye huyu anaye watia aibu miungu yenu? Na hali wao hawasadiki kumdhukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye waeneza rehema yake!
Na ikiwa wao wanataka waletewe adhabu kwa upesi, basi ndio tabia ya binaadamu kutaka kila jambo kwa haraka. Basi enyi wenye haraka! Nitakuonesheni neema yangu duniani, na adhabu yangu Akhera. Msijishughulishe kuhimiza kitu ambacho hakina budi kuwa. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 37: "Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize." Makusudio ya kauli ya "Ishara" ni ishara za maumbile zenye kuonyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na uweza wake. Na ujuzi wa ilimu za sayansi utavumbua kwa mujibu wa itavyo nyanyuka akili ya binaadamu. Na hayo ni kwa mujibu wa miadi ilio wekwa kwa wakati wake. Kila ukifika wakati maalumu Mwenyezi Mungu hudhihirisha Ishara yake, au huwasahilishia wanaadamu njia za kuzifikilia Ishara hizo.
Lau kuwa hao walio mkufuru Mwenyezi Mungu wangeli ijua hali yao wakati watapo kuwa hawawezi kuuondoa Moto kwenye nyuso zao na migongo yao, na wala hawampati wa kuwasaidia kuuondoa, wasingeli sema wayasemayo.
Kiyama hakiwajii kwa kukitarajia kutokea kwake, bali kitawazukia kwa ghafla tu kiwababaishe, wasiweze kukirudisha, wala wao hawatapewa muhula wa kutubia na kutafuta udhuru kwa waliyo kwisha yatenda..
Na Mitume wa kabla yako yaliwapata vile vile ya kufanyiwa kejeli na makafiri katika kaumu zao. Ikawateremkia hao walio wakataa Mitume na kuwafanyia maskhara adhabu hiyo hiyo ambayo wao waliifanyia maskhara na kejeli.
Ewe Nabii! Waambie: Ni nani anaye kuhifadhini na nakama zake wakati wa usiku na mchana, na akakurehemuni na kukuneemesheni? Hapana awezae hayo. Lakini wao wanaipuuza Qur'ani ambayo ndiyo inawakumbusha ya kuwafaa na kuwalinda na adhabu.
Kwani wao wanao miungu wa kuwalinda na adhabu itokayo kwetu? Hasha! Hiyo miungu yao haiwezi kujilinda wenyewe, licha kumlinda mwenginewe. Wala hapana yeyote awezae kumlinda yeyote kati yao karibu yake au pamoja naye pindi tukitaka kumuadhibu na kumteketeza.
Sisi hatufanyi haraka kuwaadhibu hawa kwa ukafiri wao, lakini tunawapururia na kuwastarehesha katika uhai wa dunia, kama tulivyo wastarehesha baba zao kabla yao, mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je! Wanajitia upofu hawaoni yanao wazunguka wakaona kuwa Sisi tunaiendea nchi na tukaipunguza ncha zake kwa ushindi wa Waumini? Ni wao ndio wenye kushinda au Waumini ambao Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwasaidia na kuwaunga mkono? Maoni ya wataalamu juu ya Aya 44: "Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza mipaka yake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?": Aya hii ni katika Aya za miujiza ya kisayansi katika Qur'ani Tukufu. Hii inaonyesha kuwa dunia si mduwara kaamili. Na wataalamu wa sayansi hawakutamakani kupima masafa ya dunia baraabara mpaka kiasi ya miaka 250 tu takriban, walipo ingia kikundi cha mabingwa walio khusika na ilimu ya kupima marefu baina ya daraja mbili za urefu longitudes. Na hayo kwa pahala mbali mbali duniani. Katika kupima huku ikadhihiri kuwa nusu ya kati ya dunia kwenye equator inazidi kuliko nusu ya poles kwa takriban kilomita 21.5. Yaani dunia imepungua katika ncha zake, yaani katika poles. Na inajuulikana maalumu kuwa sura ya dunia na masafa yake ndio msingi katika kuchorwa kwa ramani.