Alif Lam Mim Ra - Kwa kuanzia harufi hizi ni kunabihisha muujiza wa Qur'ani, juu ya kuwa imeundwa kwa harufi hizi hizi zinazo tumiwa kwa kusemea. Na pia kuwazindua watu waisikilize. Haya yaliyo tajwa katika Sura hii ni Kitabu kilicho teremshwa kwako wewe, Muhammad, kutokana nasi, ili uwatoe watu wote kwenye kiza cha ukafiri na ujinga waendee kwenye nuru ya Imani na ilimu, kwa kusahilishiwa na Mola wao Mlezi. Na nuru hiyo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kwa kuadhibisha, na Mwenye kuhimidiwa kwa kuneemesha.
Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mwenye kuumba na kumiliki kila kiliomo mbinguni na kwenye ardhi. Ikiwa hii ndiyo hali ya Mungu wa Haki, basi makafiri, wenye kukanya, watahilikika kwa adhabu iliyo kali.
Hao ndio walio khiari uhai wa duniani kuliko Akhera, na wanawazuia watu wasifuate Sharia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotoa Sharia katika macho ya watu ili wapate kuikataa. Hao ndio wanao elezwa katika yaliyo tajwa kuwa wamepotelea mbali na Haki.
Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako, ewe Nabii, ila kwa lugha ya kaumu yake ile tuliyo mtumia, ili apate kuwafahamisha aliyo kuja nayo, na wao wayafahamu, na wayaelewe kwa wepesi. Wala si juu yake yeye kuwa lazima waongoke. Mwenyezi Mungu Mwenyewe ndiye humwacha apotee anaye mtaka kwa kuwa huyo si tayari kuitaka Haki. Na humwongoa amtakaye kwa kuwa kajitayarisha vyema kufuata Haki. Naye Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu ambaye hashindiki kwa atakalo, na ambaye anayapanga mambo yote kwa mahala pao. Basi haachi kupotea wala haongoi ila kwa hikima yake.
Na tulimtuma Musa na tukamuunga mkono kwa miujiza yetu. Tukamwambia: Watoe watu wako, Wana wa Israili, kwenye kiza cha ukafiri na ujinga uwapeleke kwenye nuru ya Imani na ilimu, na uwakumbushe vituko na nakama aliyo wapelekea Mwenyezi Mungu kaumu za kabla yao. Hakika katika kukumbusha huko zipo dalili kubwa za kuthibitisha Upweke wa Mwenyezi Mungu, zinamlingania kwenye Imani kila mwenye kuthibiti kuwa na ukamilifu wa kuweza kuvumilia balaa, na kushukuru neema. Na hii ni sifa ya Muumini.