Yaa'qub yalimtibuka moyoni mwake yale ya zamani, akayaunganisha na haya mapya. Akawaambia wanawe: Nikikukubalieni itakuwa hali yangu ni ya ajabu; kwani nikikuaminini kwa huyu ndugu yenu haitakuwa ila mfano wa pale nilipo kuaminini kwa Yusuf. Mkamchukua kisha mkarudi mkisema: Kaliwa na mbwa mwitu! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye anaye nitosheleza katika kumlinda mwanangu. Wala mimi simtegemei mtu ila Yeye, kwani Yeye ndiye Mlinzi aliye na nguvu kuliko wote, na rehema yake ni kunjufu mno, hatonipa tena machungu ya ndugu yake baada ya yale ya Yusuf.
Na wale nduguze Yusuf hawakujua kuwa Yusuf aliwatilia bidhaa zao katika mizigo yao. Walipo ifungua wakakuta mali yao, na wakaona hisani aliyo wafanyia Yusuf, wakaitumia hiyo kuzidi kumpoza moyo Yaa'qub, na kumkinaisha awakubalie kwa aliyo yataka Mheshimiwa. Wakazidi kumshikilia akubali, wakamkumbusha makhusiano yao yalio wafunga kwa baba mmoja. Wakasema: Ewe baba yetu! Unataka wema gani zaidi kuliko haya, na hayo yatayo kuwa? Haya mali yetu tumerudishiwa bila ya kuchukuliwa chochote. Basi natusafiri na ndugu yetu, na tuwaletee watu wetu mahitaji, nasi tutamchunga ndugu yetu, na tutaongeza mahitaji shehena ya ngamia kuwa ni haki ya ndugu yetu! Kwani yule Mheshimiwa kapanga kuwa kila mtu humpa shehena ya ngamia.
Waliweza wana wa Yaa'qub kumkinaisha baba yao, na maneno yao yakampata palipo. Akaacha kushikilia kumzuia mwanawe asende Misri na nduguze. Lakini moyo wake haukuwacha kuwa na haja ya kuzidi kutuzwa. Kwa hivyo aliwaambia: Sitomwacha ende nanyi ila baada ya kunipa dhamana ya nguvu. Niahidini kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtanirudishia mtapo rudi. Na wala msiache kumrudisha ila mkiangamia nyinyi au ikawa adui amekuzungukeni akakushindeni. Wakamkubalia na wakampa ahadi aliyo itaka. Na hapo tena akamshuhudisha Mwenyezi Mungu ahadi yao na viapo vyao kwa kusema: Mwenyezi Mungu anayashuhudia na kuyaona yote haya yanayo pita baina yetu.
Yaa'qub alitua kwa ahadi ya watoto wake. Kisha huruma ilimpelekea kuwausia kuwa watapo ingia Misri waingie kupita milango mbali mbali, ili watu wasiwapige kijicho, huenda wakadhurika. Akasema: Wala mimi sina uwezo wa kukulindeni na madhara. Kwani mwenye kuzuia madhara ni Mwenyezi Mungu tu, na hukumu ni yake Yeye pekee. Mimi nimemtegemea Yeye, na mambo yangu na yenu yote nimemwachia Yeye. Na juu yake Yeye peke yake wategemee wote wanao tegemeza mambo yao, kwa kumuamini Yeye.
Wale vijana wakapokea wasia wa baba yao, wakapitia milango mbali mbali. Wala hayo si kama ndiyo ya kuwazuilia madhara walio kwisha andikiwa na Mwenyezi Mungu! Na Yaa'qub akijua hayo, kwani yeye alikuwa na ilimu tuliyo mfundisha. Lakini wasia wake ulikuwa ni kwa haja aliyo kuwa nayo nafsini mwake tu, nayo ni huruma ya baba kwa wanawe ambayo ameidhihirisha katika huu wasia. Na hakika watu wengi hawana ujuzi kama alio kuwa nao Yaa'qub wakamwachia mambo yao Mwenyezi Mungu awalinde.
Walipo ingia kwa Yusuf aliwapokea kwa hishima, na khasa yule nduguye kwa baba na mama ndio akamchukua na akampa siri kwa kumwambia: Usitie shaka mimi ni nduguyo Yusuf. Basi usihuzunike kwa waliyo kufanyia wewe na waliyo nifanyia mimi.