Wawekeni wanawake waliomo edani humo humo katika nyumba zenu, kwa kadiri ya uwezo wenu. Wala msiwaletee madhara yoyote, kuwaletea dhiki katika maskani. Na ikiwa wana mimba basi watoleeni gharama za kuwakimu mpaka wazae. Wakikunyonyesheeni watoto wenu hao watalaka, basi wapeni ujira wao. Na amrishaneni mambo mazuri ya kusameheana na kuacha kutaabishana. Na ikitokea kati yenu dhiki na taabu, basi baba atafute mnyonyeshaji mwengine badala ya mama aliye achwa.
Atoe mwenye nafasi nzuri ya riziki kwa mujibu alicho kunjuliwa na Mwenyezi Mungu, na mwenye dhiki ya pato atoe kwa kadiri alicho mpa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa mujibu alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.
Na miji mingi ambayo watu wake wamefanya ujabari na wakapuuza amri ya Mola wao Mlezi na Mitume wake, tukaihisabia kwa hisabu kali kwa kuchungua kila walilo litenda na kujadiliana nao, na tukawaadhibu adhabu ya kuchusha iliyo mbaya, wakagugumia malipo maovu ya mambo yao. Na ukawa mwisho wa mambo yao ni kukhasiri kukubwa mno.
Mwenyezi Mungu amewaandalia watu wa miji ya watu walio fanya ujabari adhabu ya mwisho wa ukali. Basi tahadharini na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili sawa, ambao mnasifika kwa Imani. Amekuteremshieni mtu mwenye utukufu na cheo,
Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zenye kukubainishieni baina yaliyo kweli na ya uwongo, ili awatoe walio amini na wakatenda mema kutoka kwenye giza la upotovu kwenda kwenye mwangaza wa hidaya. Na mwenye kumsadiki Mwenyezi Mungu, na akatenda vitendo vyema atamtia katika Bustani zinazo pita kati yake mito. Watakaa humo milele. Mwenyezi Mungu kamfanyia ihsani Muumini mwema kwa kumpa riziki iliyo njema.
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye umba mbingu saba, na ardhi mfano wa hizo. Amri yake inapita kote, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni mtimilivu wa uweza, na kwamba Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.