Na wengi tumekwisha wateketeza kabla ya hawa wanao kadhibisha katika mataifa yaliyo kwisha pita. Wao walikuwa na nguvu na madaraka zaidi kuliko hawa. Wakaizunguka miji wakishughulika kuchungua na kutafuta. Je! Walipata pa kukimbilia wasiangamizwe?
Hakika kwa waliyo tendewa hao wa kaumu zilizo kwisha pita ni mawaidha kwa mwenye moyo wa kufahamu hakika ya mambo, au akasikiliza uwongofu naye akili zake anazo.
Ninaapa: Hakika tumeziumba mbingu na ardhi na viumbe viliomo baina yao katika siku sita. Na hatukupata kuchoka. Rejea mambo yaliyo khusu maana ya neno "Siku" za uumbaji katika maelezo ya kitaalamu juu ya Aya za idadi 9 mpaka 12 katika Sura ya "Fuss'ilat". 41:9-12
Ikiwa haya yamebainika, basi, ewe Mtume, yastahamilie hayo wayasemayo hao wanao kanusha, ya uwongo na uzushi kukhusu Utume wako. Nawe mtakasishe, Msabbih, Muumba wako na Mlezi wako na kila upungufu, ukimhimidi wakati wa alfajiri, na wakati wa alasiri, kwani ibada nyakati hizo ni jambo kuu.
Na sikiliza khabari ninazo kwambia katika hadithi za Kiyama kwani shani yake ni kubwa. Siku atapo nadi Malaika wa kunadi kutoka pahala pa karibu na hao wanao itwa.
Siku itakapo wapasukilia ardhi, na watoke humo mbio mbio wakikimbilia mkutanoni...Hilo jambo kuu la kuwakusanya wote ni dogo na jepesi kwetu.
Sisi tunajua kuliko yeyote hayo wayasemayo ya uwongo juu yaliyo khusu Utume wako. Wala wewe hukutumwa uwalazimishe kwa unayo yataka. Ila wewe ni mwonyaji basi mkumbushe kwa Qur'ani Muumini mwenye kuiogopa adhabu yangu ili ukumbusho umfae..