Enyi mlio amini! Msitangulie na kulikata jambo lolote la kidini na la kidunia bila ya kukuamrisheni Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na jiwekeeni kinga ya nafsi zenu isikupateni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata sharia yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia baraabara yote mnayo yasema, ni Mwenye kuyajua vilivyo mambo yote.
Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu juu ya sauti ya Nabii anapo sema na nyinyi mnasema. Wala msipambanishe sauti zenu na sauti yake, kama mnapo semezana nyinyi kwa nyinyi, kwa kuchelea visiharibike vitendo vyenu bila ya nyinyi wenyewe kutambua.
Hakika wanao teremsha sauti zao katika baraza ya Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kumtukuza yeye, hao peke yao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Kwa wengineo si hivyo. Nao watapata msamaha mkubwa kufutiwa madhambi yao, na thawabu zilizo fika ukomo wa kufika kwake.
Hakika hao wanao kuita kwa makelele nawe uko vyumbani mwako wengi wao hawafahamu yanayo takikakana kukuhishimu na kukutukuza kwa makamo yako.