Wale walio kufuru, mali yao na wangayatoa kuwa ni fidia hayatowafaa kitu, wala watoto wao na wangawataka msaada hawatoweza kuwasaidia hata chembe kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu katika Akhera. Na hawa ndio walio lazimika kuingia Motoni na waselelee humo.(wadumu)
Hakika hali ya wanacho kitoa makafiri duniani kuwa ni sadaka au cha kuwakaribisha mbele ya Mwenyezi Mungu Akhera mfano wake, kwa kuwa ni kazi bure katika ujira wa vitendo, ni kama hali ya shamba la watu walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi. Shamba hilo likakumbwa na upepo wenye baridi kali ya barafu, likateketea shamba lote kuwa ni malipo yao. Wala Mwenyezi Mungu siye aliye wadhulumu ujira wa kazi yao, lakini ni wao wenyewe ndio walio jidhulumu nafsi zao kwa kufanya yaliyo sabibisha hayo. Nayo ni kuzipinga dalili na ushahidi wa Imani na kumkufuru Mwenyezi Mungu.
Enyi mlio amini! Msitafute kuwafanya marafiki wa ndani watu wasio wa Dini yenu mkatumai msaada kwao, na mkawa mkiwapa siri zenu. Hao hawatoacha kuyafisidi mambo yenu, kwani wao wanapenda mno kukutieni taabuni na kukudhuruni kwa madhara makubwa. Zimekwisha dhihiri ishara za bughdha yao kukuchukieni nyinyi katika kuropokwa ndimi zao. Na yaliyo ficha nyoyo zao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kuonyesheni alama za kumtambua rafiki na adui kama nyinyi ni watu wa akili na utambuzi wa kweli.
Enyi nyinyi Waumini! Mnawapenda hawa makafiri na wanaafiki kwa ajili ya ujamaa, au urafiki au mapenzi tu. Na wao, lakini, hawakupendeni kwa sababu ya kuing'ang'anilia dini yao. Na nyinyi mnaamini Vitabu vyote vilivyo teremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanapo kutana nanyi hujitia imani ili kukudanganyeni. Na wakisha kuacheni huziuma ncha za vidole vyao kwa chuki na kukasirika. Ewe Nabii! Waambie: Endeleeni na hiyo chuki yenu mpaka mfe! Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyajua yanayo fichikana vifuani, na atakulipeni kwavyo.
Nyinyi mkipata neema, kama vile kushinda vitani na ngawira, wao husikitika. Mkipata msiba kama ukame na kushindwa, wao hufurahia msiba wenu. Lakini nyinyi mkisubiri juu ya maudhi yao, na mkajizuilia na kule kuwafanya urafiki mliko katazwa, basi maudhi yao na uadui wao hautakudhuruni kitu. Kwani Yeye Aliye tukuka anavijua vyema vitimbi wanavyo vifanya, wala Yeye hashindwi kukulindeni nao.
Na hebu taja Ewe Nabii! Pale ulipo toka asubuhi mapema ukaacha ahali zako, watu wako wa nyumbani, ukenda mpaka Uhud kwa makusudi ya kuwaweka Waumini katika makao yao kwa ajili ya vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia kauli zenu, ni Mwenye kuzijua niya zenu.