Na kumbukeni mlipo kuwa bondeni ng'ambo hii ya karibu na Madina, na wao makafiri wako ng'ambo ile ya mbali, na msafara wenye bidhaa mlio kuwa mnautaka uko karibu zaidi nanyi upande wa baharini. Na lau kuwa mmepeana miadi ya kukutana kwa kupigana basi msinge wafikiana hivyo. Lakini Mwenyezi Mungu kapanga mkutane bila ya miadi, na bila ya kutaka wao, ili apate kutekeleza jambo ambalo katika ujuzi wake limekwisha thibiti litokee tu, wala hapana jenginelo. Jambo lenyewe ni kuwa vitokee vita vitavyo pelekea nyinyi mshinde na wao washindwe. Ipate kuondoka shaka - wateketee wa kuteketea kwa hoja wazi ya kuonekana, nako ni kushindwa makafiri juu ya wingi wao; na wahuike Waumini kwa hoja iliyo wazi, nako ni kushinda kulio toka kwa Mwenyezi Mungu kuwapa Waumini wachache. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na kujua. Haimfichikii kauli wala niya yoyote ya pande zote mbili.